China yajitosa vita vya ujangili

09Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Mikumi
Nipashe
China yajitosa vita vya ujangili

UBALOZI wa China nchini, umeunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya ujangili kwa kuziwezesha jamii zinazoishi karibu na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi pembejeo za kilimo.

Pembejeo hizo zimetolewa kwa ajili ya kuzijengea jamii hizo uwezo wa kulima kisasa ili kuwasaidia kuacha kujihusisha na vitendo vya ujangili.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu alisema hayo jana wakati Ubalozi wa China nchini ukikabidhi msaada wa pembejeo hizo kwa wananchi wa kijiji cha Mhenda, Kilosa mkoani Morogoro.

Msaada huo ni mbegu za mahindi kilo 2,500, mbegu za alizeti 150 na mbegu za choroko kilo 800. Ubalozi huo pia umetoa jozi 13 za sare za ulinzi shirikishi, buti 13, komputa mpakato nne na runinga moja

Kanyasu alisema lengo la vifaa hivyo ni kuwasaidia wananchi kujikita katika kilimo cha kisasa kwa kutumia mbegu zenye ubora wa hali ya juu.

Akizungumza katika mkutano huo, Kanyasu alisema vifaa hivyo vitatumika katika kutoa elimu kwa wananchi katika mapambano dhidi ya ujangili.

Katika hatua nyingine, Kanyasu aliipongeza Jamhuri ya Watu wa China kukomesha soko la meno ya tembo na kuamua kutoa msaada kwa wanavijiji ili kuachana na biashara hiyo haramu.

Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke, alisema pembejeo za kilimo walizozitoa zitakwenda sambamba na mafunzo yatakayotolewa na wataalam kutoka China watakaowafundisha wanakijiji kulima kwa kisasa ili kuachana na ujangili.

Alisema Ubalozi wa China umeamua kuanza na kijiji hicho ili kuwasaidia wananchi kuzalisha mazao mengi ili wasiweze kujiingiza katika vitendo haramu.

Wang alisema China imeamua kuisaidia Tanzania katika vita dhidi ya ujangilli kwa vile watalii wanakuja nchini kwa ajili ya kuangalia wanyama, hivyo vitendo hivyo vinakwamisha juhudi za serikali katika kuleta maendeleo.

Naye Diwani Mhenda, Ali Athumani, alimshukuru Balozi wa China kwa msaada huo na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi kwa vijiji vingine vilivyo karibu na hifadhi hiyo.

Habari Kubwa