China:Tuheshimiane,kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine

19Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
China:Tuheshimiane,kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine

China imetoa wito kwa mataifa mengine duniani kuheshimiana na kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio chochote kile na kueleza kuridhishwa kwake na namna mchakato wa uchaguzi mkuu unavyoendelea hapa nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na
Balozi wa China hapa Nchini. Wang Ke wakati walipokutana
kwa mazungumzo leo Jijini Dar es Salaam

Kauli hiyo imetolea na Balozi wa China Nchini, Wang Ke leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na kuongeza kuwa ni lazima Mataifa yote yaendeleze mahusiano mema miongoni mwao na kutoingilia masuala ya ndani ya Mataifa mengine. 

 

Aidha Balozi Wang Ke ameongeza kuwa China itaendelea kuheshimu masuala ya ndani ya Mataifa yote Tanzania ikiwemo na kueleza kuridhika kwake na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea nchini na kuwatakia Watanzania kila la heri katika uchaguzi huo.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema  ushirikiano iliopo baina ya Tanzania na China kisiasa, kiuchumi na kijamii ni madhubuti na imara na kwamba Tanzania itaendelea pia kuheshimu mashirikiano na mataifa mengine. 

 

Aidha Katibu Mkuu Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati kwa Tanzania na kwamba uhusiano huo utaendelea kudumishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.

Habari Kubwa