Chongolo aonya viongozi TASAF

14Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Chongolo aonya viongozi TASAF

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewataka viongozi wa umma kuacha tabia ya kujineemesha na pesa za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) zinazotolewa kwa ajili ya watu wasio na uwezo wa kumudu maisha yao.

Chongolo amesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya viongozi wa umma kujiingiza kwenye mfuko huo  wa TASAF kama walengwa pidi wanapostaafu.

“Siku hizi imekuwa fasheni, mtu akifikisha miaka sitini anasema na mimi mlengwa wa TASAF, mlengwa wa zile fedha ni watu wasio na uwezo wa kumudu maisha yao, tusiende kujineemesha sisi , tusiende kujitengenezea ulaji sisi, ziache ziende kwa walengwa,” amesema.

Chongolo ametoa maagizo hayo leo wakati akiongea na viongozi wa serikali ya Mkoa wa Kagera pamoja na wanachama wa CCM alipofika yeye pamoja na wajumbe wengine wa Secretarieti ya Halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama pamoja na kukagua uhai wa chama ngazi ya mashina.

Katika hatua nyingine Chongolo amewataka viongozi wa serikali Mkoani humu kuhakikisha asilimia 10 ya mapato ya mkoa huo yanaenda kwa wakati kwa vijana, akina mama pamoja na walemavu kama ilivyopangwa ili kuwawezesha watu hao kupata mitaji kwa ajili ya maendeleo yao.

“Hizi fedha ni muhim sana kuzitenga na kuzitoa tena kwa wakati kwa sababu vijana, akina mama na watu wenye ulemavu wanahitaji fedha hizi kuwa mitaji kwa ajili ya shughuli zao,” amesema.

Chongolo ametoa kauli hiyo baada ya  kupokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Kagera ambapo alielezwa kuwa mkoa huo umetoa shilingi milioni 438 Kati  asilimia 10 ya mapato  yanayokwenda kwa akina mama, vijana na wenye ulemavu.

Katika hatua nyingine Chongolo amesisitiza Chama kuendelea kusimamia kila fedha iliyopangwa kwa ajili ya maendeleo inashuka kwa wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa.

"Bajeti ya mkoa kwa mwaka 2021/22 ilikuwa bilioni 294, mpaka sasa zimeshashuka zaidi ya bilioni 60, lakini Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ameshusha Shilingi bilioni 20 mkoa wa Kagera kwa ajili ya maendeleo kama vile miundombinu ya elimu na afya kwa lengo la kuwaondolea wananchi kero ya kuchanga michango kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kama ilivyokuwa hapo awali, na hizi ni fedha za ziada nje ya bajeti ya mkoa."

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa "Kazi yetu sasa kama Chama ni kuhakikisha fedha hizo hazipotei hata senti moja, 'kutoa jicho' na sisi tumekuja hapa timu nzima, lengo letu kupita kila eneo kuhakikisha kila senti iliyoshuka haipotei na inakwenda kutafsiri matokeo halisi ya maendeleo kwa wananchi."

Aidha, Katibu Mkuu ameeleza pia lengo la ziara hii ni kuhimizana, kuhamasishana na kukumbushana taratibu za Chama chetu, ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama chetu unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Ndg. Constansia Buhiye ameishukuru Sekretarieti ya Halmshauri Kuu ya CCM Taifa kwa ziara hii, kwani itaendelea kuhamasisha maendeleo na uhai wa Chama mkoani humo.

Habari Kubwa