Chuo cha Uhasibu Arusha kuunganisha wananchi Afrika Mashariki

04Dec 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Chuo cha Uhasibu Arusha kuunganisha wananchi Afrika Mashariki

MKUU wa Chuo cha Uhasibu (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeki amesema chuo hicho, kimejipanga kutumia sekta ya elimu kuwa kiungo cha kuwaunganisha wananchi wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Prof.Eliamini Sedoyeki akitoa zawadi kwa washindi katika mdahalo wa kujadili muelekeo wa taasisi hiyo.

Hayo ameyasema leo katika kusanyiko lililowaleta pamoja wanafunzi waliowahi kusoma IAA lililofanyika katika ukumbi wa papa chuoni hapo sambamba na kujadili mada na kuunda umoja wa wanachuo waliowahi kusoma chuoni hapo, ambapo wanafunzi hao walitoa  zawadi kwa wanafunzi waliopo chuoni hapo waliofanya vizuri katika masomo.

Amesema muda muhafaka kwa taasisi za elimu nchini kuangalia wapi walipotoka na wanapoelekea kwa kujenga mahusiano mazuri.

Hata hivyo, amesema chuo hicho, kama sehemu ya kitivo cha diplomasia mkoani hapa, wajipanga kutumia mafunzo ya elimu chuoni hapo kuwaunganisha watu kutoka ukanda wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa kitu kimoja.

"Chuo chetu kipo Arusha sehemu ya kitivo cha kidiplomasia na Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tumejipanga kutumia sekta ya elimu kuwaunganisha watu kutoka nchi za Afrika Mashariki kuwa kitu kimoja,"amesema Sedoyeki.

Amesema chuo hicho, kimeweka mpango mkakati wa kuboresha mazingira ya wanafunzi kusomea kwa kujenga miundombinu ya madarasa ya kisasa, kuongeza kozi mbalimbali na kuboresha mazingira  ya watumishi kufanya lazi. 

Aidha amesema chuo hicho,kimefanya mazungumzo na Chuo Kikuu cha Bujumbura (Burundi), ili wakafundishe kozi mbalimbali zinazofundishwa IAA.

Amesema wakipata fursa ya kwenda kufundisha kozi hizo nchini, Burundi itaisaidia nchi hiyo kuwa na bodi itakayojitegemea.

Licha ya kuzungumza hayo, amesema wamefanya mazungumzo na uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki chuo cha IAA, kipate fursa ya kwenda nchi ya Sudan Kusini kufundisha kozi mbalimbali kwa kuwa nchi hiyo bado ni changa kielimu.

Amesema endapo watapata fursa hiyo, lengo la chuo hicho ni kutoa mafunzo bora ambayo yatazalisha wataalamu kwenye nchi hizo.

"Sisi kama taasisi bora Afrika tunatoa kozi za fedha,biashara ma tehama hivyo tumeanza kuangalia fursa zilizopo kwenye nchi hizo kwa ajili ya kuwapatia ujuzi,"amesema Sedoyeki.

Amesema chuo hicho, kimeanza utaratibu wa kuboresha miundombinu ya madarasa na mfumo tehama na hadi sasa amesema wamesha nunu kompyuta 100 na kuangiza nyingine 300.

" Miezi sita ijayo tumepanga kuongeza madarasa 24, kumbi za mikutano za kutosha ili wanafunzi wasome katika maeneo yenye hadhi ya kimataifa .

Rais wa kusanyiko la wanafunzi waliosoma chuoni hapo, Dk.Edson Lugua, amesema baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi hatahakikisha anawaunganisha wasomi waliosoma chuoni hapo kuwa kitu kimoja, kwa kujadili mambo muhimu kwa maslai ya taasisi hiyo na taifa kwa ujumla.

"Lengo la mdahalo huu ni kuwaleta wasomi waliosoma chuoni hapa, pamoja na wafanyakazi kuweka mpango mkakati wa kuendeleza taasisi hii kupiga hatua ya kimaendeleo.

Habari Kubwa