Chupa 100 za damu zinatarajiwa kukusanywa kwa siku

21Sep 2020
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
Chupa 100 za damu zinatarajiwa kukusanywa kwa siku

Benki ya damu salama inatarajia kukusanya chupa 100 za damu kwa siku katika wiki ya ukusanyagi wa damu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliyoanza leo Septemba 21 na kukamilika Septemba 25 mwaka huu.

Lengo la zoezi hilo ni kuokoa maisha ya mama na mtoto, majeruhi wa ajali na wagonjwa wenye uhitaji wa kuongezewa damu.

Mkuu wa Kitengo cha  kuchangia Damu Nyanda za juu kusini, Bahati Tembo amesema hayo leo Septemba 21, 2020 wakati wa zoezi la wiki la uchangiaji damu, ambapo amesema wanalenga kuokoa maisha ya mama na mtoto,  majeruhi wa ajali mbalimbali pamoja na  wagonjwa wengine wenye mahitaji ya damu.

Bahati amesema wiki la uchangiaji damu mwaka huu limeamua kulifikia kundi la Askari mgambo kwa sababu lina watu wengi na wanafikika kirahisi na kwamba wamefikia umri wa kuanzia miaka 18  ambayo ni sifa moja wapo inayohitajika katika kuchangia damu.

“Mwaka huu katika wiki ya uchangiaji damu tumeamua kuwafikia askari mgambo kwa sababu ni kundi ambalo linajitolea kwenye masuala mbalimbali tutafika kila makambi ya askari mgambo ili kukusanya damu kwa wingi ili kuweza kuokoa wamisha ya watanzania wenzetu,” amesema Tembo.

Ameongeza kuwa jumla ya Askari Mgambo 1000 kwa Mkoa wa Mbeya wanatarajiwa kuchangia damu na kwamba kwa siku watahakikisha wanakusanya uniti 500 ambazo ni sawa na chupa 100 za damu katika kila Wilaya watakayofika.

Akizungumzia mwitikio wa wananchi kuchangia damu, amesema ni mdogo na kwamba wananchi wa Mkoa wa Mbeya ni wabishi kushiriki zoezi hilo licha ya kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuchangia damu.

Ameongeza kuwa mwaka huu hawaweza kulifikia kundi la wanafunzi hususani wa Sekondari kwa sababu wengi wao wanajiandaa na mitihani lakini pia asilimia kubwa ya wanafunzi hawajafikia umri wa miaka 18 ukilinganisha na askari mgambo ambao wengi wamevuka umri huo.

Baadhi ya askari mgambo ambao walishiriki zoezi la kuchangia damu, Charles Mgogo kutoa eneo la sabasaba amesema ameamua kuchangia  damu kwa sababu ya kuokoa maisha ya mama na mtoto na kwamba  utayari huo unaweza kuwa fadhila na kwake pindi atakapopata matatizo.

Amewahamasisha wananchi kuendelea kuchangia damu kwa madai kuwa mahitaji bado ni makubwa na wataoweza kuokoa maisha ya wenzao ni wale ambao wanasifa ya kuchangia.

Mustafa Mgweno amesema yeye ni mara ya kwanza kuchangia damu na alishawishika kufanya hivyo mara baada ya kupewa elimu juu ya faida za kuchangia damu kutoka kwa wataalam wa kitengo hicho walipowatembea.

Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wenye Ulemavu Kitengo cha Damu salama mwaka 2020 kimelenga kukusanya chupa 32,700 huku timu za mikoa ni chupa 150, timu za damu salama vituo vya kanda chupa 500 Hospitali za Kanda  chupa 150.

Habari Kubwa