'Chupi' akamatwa Msumbiji apanda kizimbani Lindi

22Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
'Chupi' akamatwa Msumbiji apanda kizimbani Lindi

MFANYABIASHARA wa duka katika kata ya Chamazi, wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, Mateso Albano au Mateso Chupi (39) aliyetoroka chini ya ulinzi na kwenda kuishi Msumbiji muongo mmoja uliopita, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Lindi mkoani hapa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Chupi anakabiliwa na shitaka la kukutwa na vipande sita vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh. 67,365,000 isivyo halali.

Chupi alipanda kizimbani mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Mussa Ngaru, Ijumaa na kusomewa shtaka linalomkabili na wakili wa serikali, Abdulrahaman Mohammed.

Mshitakiwa Chupi alidaiwa kukamatwa na vipande sita vya meno ya tembo katika kituo cha kuuzia mafuta mjini Liwale Septemba 27, 2008, lakini akafanikiwa kuwatoroka polisi na kwenda kuishi nchi jirani ya Msumbiji.

Chupi alikamatwa Msumbiji Jumanne iliyopita.

Akisomewa shtaka linalomkabiri mbele ya Hakimu Ngaru, wakili wa serikali Mohammed alidai mshitakiwa alikamatwa na polisi akiwa na vipande hivyo sita Septemba 27, 2008, akiwa tayari kuvisafirisha kuelekea kutafuta soko.

“Mheshimiwa hakimu huyu mshitakiwa alikutwa eneo la kituo cha kuuzia mafuta pale Liwale mjini akijiandaa kwa safari, lakini kabla ya kuondoka alikamatwa na askari polisi,” alisema wakili huyo.

Mwanasheria huyo alidai kuwa mshitakiwa ambaye hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri lake kisheria, alifanya kosa chini ya Sheria ya Uhifadhi Wanyama ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Chupi amepelekwa rumande na kesi hiyo itatajwa tena katika mahakama hiyo Januari 31, mwaka huu. 

Habari Kubwa