Corona ilivyoibua ukiukwaji wa mtaala wa elimu shuleni

21Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Corona ilivyoibua ukiukwaji wa mtaala wa elimu shuleni
  • *Pia kiulizo haki za walimu kisheria

​​​​​​​VIRUSI vya corona vilivyoripotiwa kulipuka Wuhan, China Desemba 2019, vimekuwa na madhara karibu kwa kila sekta ulimwenguni.

Waziri wa elimu Profesa Joyce Ndalichako.

Hadi jana saa saba mchana, mtandao wa Worldmeters ulionyesha kulikuwa na watu 96,701,903 waliopata maambukizo huku 2,067,951 wakifariki dunia kutokana na virusi hivyo.

Nchini kumebainika kuwapo ukiukwaji mkubwa wa kanuni na miongozo ya taaluma kwa baadhi ya shule za binafsi, zinazobadilisha taratibu wa ufundishaji ili kufidia muda uliopotea wakati wa mlipuko wa virusi hivyo.

Nipashe imebaini baadhi ya wanafunzi, hasa wanaokabiliwa na mitihani, wanakalishwa darasani wakifundishwa kuanzia alfajiri hadi usiku.

Pia adha hiyo ya muda wa ziada unagusa kufutwa kinyemela kwa mapumziko ya wikiendi, siku ya Jumamosi na baadhi ya shule hata Jumapili, kufanywa kuwa za mahudhurio darasani.

Udadisi wa Nipashe katika baadhi ya shule za jijini Dar es Salaam umebaini mpango wa muda wa ziada unatokana na kufidia miezi mitatu (wiki 13 au wastani saa 78), ambao watoto hawakuwapo masomoni kutokana na mlipuko wa maradhi ya corona Machi, mwaka jana.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo binafsi (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya, akizungumza na gazeti hili, anatetea nyongeza ya muda huo kwamba ni kufidia muda uliopotea wa masomo, kutokana na adha ya corona.

“Mwanafunzi anatakiwa kukaa siku 194 kwa mwaka, zimepungua mwaka jana (2020) kutokana na corona, hii inafidia siku zilizopungua miezi mitatu.

“Wazazi wakubaliane na hiyo hali, hata kulipa ada yote mbali na shule kufungwa sababu huduma ziliendelea kwenye shule mfano ulinzi, maji,” anasema Nkonya.

Hata hivyo serikali iliagiza shule zote kuongeza muda wa saa mbili za masomo darasani kufidia muda uliopotea wanafunzi walipokuwa nyumbani.

Katika kipindi cha miezi sita ambacho walihudhuria masomo kuanzia Juni 29 mwaka jana hadi Desemba 18, ambayo inamaanisha kuondoa likizo fupi ya zaidi ya wiki moja, Agosti mwaka jana, wanafunzi wamehudhuria darasani kwa wastani wiki 22.

Kwa kuzingatia mahudhurio shuleni ya siku tano kwa wiki, wanafunzi wamekaa darasani kwa siku 110, ambayo kila siku ya masomo walikuwa na saa mbili za ziada inayowapa jumla ya saa 220 wakati zilizopotea kwa corona zilikuwa saa 78, hivyo kuna ziada isiyopungua saa 140, sawa na wiki 20.

Uchunguzi wa Nipashe, uliozuru katika shule mbalimbali za wilaya za Kinondoni, Ubungo, Ilala na Temeke, umebaini msukumo mkuu nyuma ya pazia kwa tishio hilo la kiafya kwa wanafunzi, ni ushindani wa kibiashara.

Baada ya kubainika ufaulu ndiyo mvuto mkuu wa soko kwa shule, nazo kutokana na ushindani mkubwa uliopo, zimejikuta zikitumia mbinu kwa mfumo wa kuigana kibiashara.

Uchunguzi wa Nipashe, baadhi ya shule zilizoko maeneo ya Ubungo, Kimara, Ukonga, Mbezi Beach, Tabata, Segerea na Mbagala, umebaini wanafunzi wengi wa darasa la saba na la nne wamekuwa wakiingizwa darasani kuanzia alfajiri hadi kati ya saa mbili na saa tatu pasipo kurudishwa bwenini.

Shule nyingi zimegundulika kuwalazimisha wanafunzi wa madarasa yanayokabiliwa na mitihani, zaidi darasa la nne na la saba, pia kidato cha pili na cha nne wanahamishiwa mabwenini kwa malipo ya ziada maradufu.

Ni hatua ambayo baadhi ya wazazi waliohojiwa na Nipashe, akiwamo Bryson Eliezer na Hilda Mosha (majina ya watoto wao na shule wanakosoma tunayo), wamethibitisha wameshawishiwa kupeleka bwenini watoto wao, ili wakasaidiwe kwa karibu kitaaluma, pasipo kuwekewa wazi mengine yanayojiri kuhusu ratiba.

MAELEKEZO YA KISERIKALI

Ratiba hiyo inapingana na maelekezo kutoka Mtaala wa Elimu ya Msingi wa Mwaka 2007, unaoweka wazi muda wa kusoma au kujifunza kwa aliyeko kuanzia darasa la tatu hadi la saba, ukomo wake ni saa sita kwa siku.

Aidha, serikali inaelekeza kwa wanafunzi walioko katika madarasa ya kwanza na la pili, wasizidishe saa tatu na nusu (3½) kila siku.

Vivyo hivyo, serikali inaelekeza kila mwaka wa masomo utakuwa  mihula miwili itakayokuwa na majuma 21 kwa kila muhula.

Hiyo inamaanisha kila muhula utakuwa na jumla ya siku 147, ambayo ni sawa na wastani wa miezi mitano kasoro siku kadhaa.

Hali kadhalika, ikirejewa maagizo ya mwanafunzi wa darasa la tatu hadi la saba, anatakiwa kukaa muda wa saa sita akisoma na kujifunza, kwa anayeingia asubuhi walau hadi saa tisa muda wake utakuwa umeisha, tena kwa maelekezo ya kati ya Jumatatu hadi Ijumaa.

Serikali inaelekeza kila wiki madarasa ya tatu hadi saba, ambayo yanaangukia kwenye makundi ya mitihani, yatakuwa na jumla ya vipindi 42 yenye dakika 40 kila kimoja.

Lakini kwa kile Nipashe imekibaini, ufundishaji umefikisha si chini ya vipindi 84 hadi 90 kwa wiki.

SHIDA YA AFYA

Daktari wa Binadamu, Pedro Pallangyo, akizungumza na gazeti hili, anasema kiafya saa za kukaa darasani kwa mtoto aliye shule ya msingi zisizidi 12.

“Kila kitu kina kipimo chake, saa 12 kwa mtoto wa shule ya msingi, hapana! Ubongo hauwezi kupokea kwa saa zote hizo,” anasema Dk. Pedro.

Mtaalamu wa Lishe, Theresia Thomas, ana msisitizo wake kuhusu hilo kwamba kadri mwanafunzi anavyotumia muda mrefu katika masomo darasani, atahitaji chakula kilicho na nishati ya kutosha kipindi cha mapumziko.

“Kikubwa nishati lishe inahitajika kuzingatiwa kwa mtoto yeyote. Iwapo mzazi ataona ni vyema akamfungashia mtoto wake juisi au matunda, ili akipata muda ale, muda wa mapumziko itafaa na si kusoma saa nyingi bila mlo, uelewa unachangiwa na lishe,” anasema Theresia.

Msaikolojia Tiba, Saldin Kimangale, anasema kumrundikia mtoto mambo mengi, anaangukia kupata msongo wa mawazo na hofu, inayomwondoa hatimaye katika hamasa na kufurahia masomo.

“Kumjazia mtoto mambo mengi na hasa ratiba zao za shule kiasi cha kukosa wakati wa kucheza na kufurahi ni kasoro katika malezi bora.

Mtaalamu huyo, anataja athari anazoweza kuzipata kutokana na kujaziwa mambo mengi kwa wakati mmoja ni pamoja na kupoteza vipaji na ubunifu alivyonavyo.

“Afya ya mwili ya mtoto pia huathirika, na kama tujuavyo afya ndio rasilimali na mtaji wa kila tunachofanya,” anakumbusha mtaalamu huyo. 

SHERIA YA MTOTO

Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, inatamka wazi kwamba wazazi   hawana   budi   kuwapeleka   watoto shuleni  na  kuwapa  nafasi  ya  kucheza  na kupumzika.

Wakati kukiwa na ukukwaji wa haki za wanafunzi kwa kukalishwa darasani muda wa ziada kuanzia mapema asubuhi hadi usiku kati ya saa tatu na nne kwa shule nyingi za watu, nako kumezaa kiulizo kwenye haki za walimu wanaowafundisha.

Wakati inaelekezwa kisheria wanafunzi wanapaswa kuhudhuria masomo kwa wastani wa muda usiozidi saa saba, Sheri ya Ajira na Uhusiano Kazini, iliyoanza nchini mwaka 2004, inaweka wazi muda wa mfanyakazi kutumika ni saa tisa kwa siku.

Vilevile, ina ufafanuzi pindi inapotokea muda wa ziada, usizidi saa mbili na nusu. Lakini, inaporejea uhalisia wa kilichotokea baada ya mlipuko wa corona na kinachoendelea sasa baada ya shule kufunguliwa, ratiba za masomo zinachukua saa 14 kwa siku.

Ni mustakabali unaozua kiulizo kuhusu 'utii bila shuruti' wa sheria za nchi, waraka rasmi na maelekezo ya kiserikali, hata wanafunzi wakakaa darasani mara mbili ya muda uliolekezwa na serikali, huku walimu wao wakiwa na wastani wa ziada ya saa tatu hadi nne kazini.

KAULI YA WAZIRI ELIMU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, hivi karibuni katika mkutano mkuu wa mwaka wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania Bara (TAHOSSA), ana hoja inayojibu kinachojiri.

“Kumeibuka tabia ya shule imesajiliwa kama ya kutwa mara ya muda kidogo inakuwa ya bweni bila hata kufuata taratibu eti tuu kwa sababu imejenga 'kajengo kamoja na kukaita' bweni.

“Darasa la mitihani ndiyo walimu wanaona ndilo la kumjazia mtoto vitu vyote, unakuta hata shule hawafungi eti tu kwa sababu ya mitihani kwa nini hali hiyo isiwe toka madarasa mengine ya chini na siyo kusubiri wakati wa mitihani?” Anahoji Ndalichako.

Agizo la Prof. Ndalichako, ambaye ni mtaalamu bingwa wa mitaala, anazitaka shule binafsi zirejee na kuhakikisha hazitoki nje ya kanuni za usajili wao na kuacha tabia ya kujichukulia hatua bila kuishirikisha serikali.

Vivyo hivyo, anaelekeza kidole cha kung’aka dhidi ya tabia za shule kusubiri darasa la mitihani, ndiyo wanahamia utaratibu wa kuwalimbikizia masomo wanafunzi.

Habari Kubwa