CRDB yatoa msaada wa chakula kwa watoto yatima wa kiislam

22May 2020
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
CRDB yatoa msaada wa chakula kwa watoto yatima wa kiislam

BENKI ya CRDB Tawi la Mpanda mkoani Katavi, Iimetoa msaada wa chakula kwa watoto yatima wa dini ya kiislam waliopo katika Manispaa ya Mpanda mkoani humo kwa ajili ya sikukuu ya Eid.

Meneja wa CRDB akigawa chakula kwa watoto yatima.

Akikabidhi msaada huo leo kwa Shekh Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meneja wa benki hiyo Tawi la Mpanda, Hamad Masoud, amesema watoto hao wanahaki ya kufurahia sikukuu ya Eid kama walivyo watoto wengine ambao wana wazazi wao.

Masoud amewataka watoto hao kutojiona hawana thamani katika Dunia, hivyo inabidi wasome kwa bidii huku wakiondoa fikra hizo kwani kuna watu wanahistoria kubwa katika maisha yao na sasa ni watu wakubwa hapa Duniani.

Watoto

"Yawezekana ukawa unajiona upo katika mazingira magumu sana, yawezekana ukawa umekata tamaa sana, yawezekana ukajiona wewe hapa Duniani hufai, lakini mimi niwatie moyo na mjuwe kuwa Mwenyezi Mungu ndiyo mtoa riziki," amesema Masoud.

Kwa upande wake, Shekh Mkuu wa Mkoa huo, Mashaka Kakulukulu, ameishukuru benki ya CRDB kwa kufanya tukio hilo muhimu la kuwakusanya watoto na kuwapa zawadi kwa ajili ya Eid kama vitabu vya dini vinavyo elekeza.

Amesema hiyo iwe ni ishara kwa Taasisi zingine au mtu mmoja mmoja kuiga mfano huo uliyo fanywa na benki hiyo na kujuwa kwamba wanao wajibu wa kuwalea watoto hao kwani wao hawakupenda kuondokewa na wazazi wao.

Shekh Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu, akizungumza baada ya kupokea msaada huo.

Hata hivyo, watoto waliopewa msaada huo pia walitoa shukurani zao kwa benki hiyo na uongozi wa Bakwata kwa ujumla kwa kuwajali na kuwakumbuka katika kipindi hiki cha Eid hivyo waliomba waendelee kuwasaidia na kuwalea katika mazingira ya dini.

Habari Kubwa