CUF yaanza maandalizi ya uchaguzi

19Jun 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
CUF yaanza maandalizi ya uchaguzi

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeanza kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho na wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa kuitisha kongamano jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Abdul Kambaya.

Chama hicho kimeanza maandalizi hayo kwa kufanya kongamano la uzinduzi wa sera na kaulimbiu mpya ya chama hicho Jumamosi jijini Dar es Salaam.

Katika taarifa yake kuhusiana na  kongamano hilo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Abdul Kambaya, alisema uzinduzi wa sera hiyo mpya utafanywa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba.

Kambaya alisema katika uzinduzi huo, wamekaribisha watu mbalimbali bila kujali itikadi za vyama vyao.

“Kongamano hili limepewa jina la ‘Sauti ya haki na furaha kwa Watanzania wote’. Kongamano hilo litahudhuriwa na wanachama wa CUF wakiongozwa na viongozi wao wakuu, uzinduzi wa sera hizo ni katika kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na wa Serikali za Mitaa ambao utahusisha mitaa, vijiji na vitongoji ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu,” alisema Kambaya.

Aliongeza: “Na uzinduzi huu unafanyika mara tu baada ya kumalizika kwa kesi zilizodumu kwa takriban miaka mitatu na kusababisha baadhi ya wanachama wa CUF kufukuzwa.”

Kambaya alisema kuwa kongamano hilo sio tu litatoa mwelekeo mpya wa chama, lakini pia litatumika kuonyesha nguvu za CUF katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, na kwamba sera hiyo mpya inatarajiwa kujikita katika kutumia rasilimali na maliasili za Tanzania katika kuleta haki hizo na furaha kwa Watanzania wote.

Habari Kubwa