CUF Maalim Seif sasa yalia njaa

28Nov 2016
Richard Makore
Dar es Salaam
Nipashe
CUF Maalim Seif sasa yalia njaa

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, amesema chama hicho kwa sasa kinapitia wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yake kutokana na kunyimwa ruzuku ya karibu Sh. nusu bilioni.

Mwanasiasa huyo ambaye pia amewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesitisha ruzuku ya CUF kuanzia Agosti mwaka huu hadi sasa huku akifafanua kuwa kila mwezi walikuwa wanapata Sh. milioni 117, hivyo kwa kipindi hicho cha miezi minne, chama hicho kimekosa ruzuku ya Sh. milioni 468.

Maalim Seif alidai Msajili amewaambia amechukua hatua hiyo baada ya kuwapo kwa mgogoro wa kiuongozi ndani ya chama hicho kinachoshika nafasi ya tatu kwa kuwa na wabunge wengi.

Aidha, Maalim Seif alisema kuna vitendo vingi vinavyofanywa na dola kukihujumu chama hicho ambavyo havina uhusiano na mambo ya siasa.

Alitaja baadhi ya vitendo ambavyo havina uhusiano na siasa kuwa ni pamoja na wafuasi wa mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba, kuvunja geti la ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam na kuharibu mali huku Jeshi la Polisi likisimamia ukiukaji huo wa sheria.

Kiongozi wa CUF alitumia muda mwingi wa mkutano wake huo na waandishi wa habari kulitupia lawama jeshi hilo na Ofisi ya Msajili akiwatuhumu kuwa wanatumika kumlinda Prof. Lipumba licha ya kuwa alifukuzwa uanachama na vikao halali.

Alisema chama hicho kimekumbana na changamoto nyingi tangu Prof. Lipumba alipotangaza kutaka kurejea katika nafasi aliyokuwa nayo awali ya uenyekiti.

Prof. Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa CUF Agosti 6, mwaka jana na kuutangazia umma kwa maelezo kuwa nafsi inamsuta kuongoza chama ambacho kipo katika umoja ambao umemteua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea urais, katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

MUDA MWINGI
Lowassa alikuwa akituhumiwa kuwa fisadi na wapinzani kwa muda mwingi kabla hajatangaza kuhama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Agosti mwaka jana.

Hata hivyo, mapema mwaka huu mtaalamu huyo wa masuala ya uchumi aliibuka na kutaka arejeshewe nafasi yake.

Katika mkutano wake wa jana na waandishi wa habari, Maalim Seif alisema hivi karibuni Prof. Lipumba alivamia mkutano mkuu wa chama hicho uliokuwa unafanyika jijini Dar es Salaam, lakini hakuchukuliwa hatua yoyote na polisi badala yake alilindwa pamoja na matukio mengine anayoyafanya katika ofisi mbalimbali za chama hicho nchini.

Alitaja matukio mengine kuwa ni pamoja na kutekwa kwa viongozi wa chama hicho wanaompinga Prof. Lipumba, polisi kuzuia mikutano mbalimbali ya chama hicho ambayo yeye (Maalim Seif) anapangwa kuhutubiwa.

Kuhusu kiini cha mgogoro ndani ya chama hicho, Maalim Seif alisema mpaka sasa Prof. Lipumba hajasema sababu kuntu iliyomfanya ajiuzulu mwaka jana huku akieleza msomi huyo ndiye mwasisi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Maalim Seif alisema Prof. Lipumba akiwa katika Bunge Maalum la Katiba pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa vinavyounda Ukawa (Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD) walikubaliana na kuanzisha umoja huo.

Alidai sababu zilizotolewa na Prof. Lipumba wakati anajiuzulu mwaka jana siyo za kweli kwa yeye ndiye aliyefanya utafiti na kubaini kwamba aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Lowassa anakubalika na hivyo akapendekeza ateuliwe kuwa mgombea.

Alisema yanayokikumba CUF kwa sasa ni mapito na kwamba ipo siku haki itaibuka na kuwataka wafuasi na wapenzi wa chama hicho kuwa na subira.

Alipoulizwa sabbu za kutojibu barua ya Prof. Lipumba aliyomwandikia wakati alipojiuzulu, Maalim Seif alisema alikuwa anasubiri kuitishwa kwa mkutano mkuu.

Alisema Katibu Mkuu hana mamlaka kwa mujibu wa katiba yao kumjibu Mwenyekiti (Prof. Lipumba) na alipoitisha mkutano mkuu ulivurugwa.

MAGARI MATANO
Katika hatua nyingine, wafuasi wa CUF wanaomuunga mkono Prof. Lipumba wamekamata magari matano yaliyokuwa yamefichwa na upande unaomuunga mkono Maalim Seif.

Akizungumza na Nipashe jana katika ofisi za CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam, msemaji wa upande wa Prof. Lipumba, Abdul Kambaya, alisema magari hayo kwa sasa yamewekwa ofisini kwao.

Alitaja magari hayo kuwa ni yenye namba za usajili T 794 BKZ, Land Cruiser, T 511 DEB Pick up, T 878 CES Land Cruiser, T 532 DEB Pick up na T 527 aina ya Land Cruiser.

Alisema magari hayo yalikutwa Kimara Bonyokwa jijini Dar es Salaam yakiwa yamefichwa nyumbani kwa mtu na kwamba hawakutaka kuendesha kesi badala yake waliyachukua na kuyarudisha ofisini.

Habari Kubwa