CUF nayo yajitoa uchaguzi wa mitaa

13Nov 2019
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
CUF nayo yajitoa uchaguzi wa mitaa

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimefuata nyayo za vyama vingine vya upinzani kwa kujitoa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kikidai mchakato wake si huru na wa haki.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba (kushoto),
akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, wakati akitoa tamko la chama hicho, la kutokushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, jijini Dar es Salaam jana.. PICHA NA JUMANNE JUMA

Kimesema kimelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya asilimia 90 ya wagombea wake katika uchaguzi huo kuenguliwa na wasimamizi wasaidizi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu msimamo wa CUF, Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba, aliitaka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutotumia nembo ya chama hicho kwenye karatasi zitakazotumika katika uchaguzi huo.

“Haki haipaswi kutendeka tu, bali inapaswa kuonekana ikitendeka katika mchakato wa uchaguzi mwanzo mpaka mwisho," Prof. Lipumba alisema.

"Kwa kuwa wagombea wetu wameshaondolewa katika ushindani kwa zaidi ya asilimia 90, sisi hatuwezi kushiriki katika uchaguzi huo. Jukumu letu kwa sasa ni kukijenga chama ili kiwe ngangari kinoma, ili tunapotoa uamuzi utekelezeke."

Kiongozi huyo wa CUF, aliwataka wagombea wa chama hicho walioteuliwa kushiriki uchaguzi huo, kuandika barua za kujitoa na kuelekeza nguvu zao kukijenga chama.

Uamuzi huo umetolewa ikiwa ni siku chache baada ya vyama vingine saba vya upinzani kutangaza kujitoa kushiriki katika uchaguzi huo kwa madai sawa na yaliyoelezwa na Prof. Lipumba jana.

Vyama hivyo ni ACT-Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NLD, Chauma, NCCR-Mageuzi na UPDP na Chama Cha Kijamii (CCK).

Habari Kubwa