CUF: Tumechoshwa na unyanyasaji

26Feb 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
CUF: Tumechoshwa na unyanyasaji

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kimechoka kuvumilia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu wanavyofanyiwa wafuasi na viongozi wake visiwani Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wanachama wa kijiji cha Dunga, baada ya kutembelea baraza ya CUF iliyovunjwa na kuchukuliwa bendera za chama hicho.

Alisema licha ya tukio hilo, kuna matukio mengi ya udhalilishaji na uvunjwaji wa haki za binadamu, wanayofanyiwa wafuasi wa CUF, likiwamo tukio la kupigwa kisha kuvuliwa nguo zote katibu wa tawi jimbo la Kojani, kisiwani Pemba.

katika tukio hilo, alisema katibu huyo alifuatwa nyumbani kwake na askari kisha kupigwa na kuvuliwa nguo zote bila kuelezwa kosa alilolifanya.

“Tumevumilia mengi akini sasa tumechoka. Nasema hili liwe tukio la mwisho, sasa tunapiga mstari mwekundu. Endapo atadhalilishwa mwanachama wetu hatukubali, hatukubalih hatukubali,” alisema.

Alisema kwa sasa CUF iko tayari kulipiza kisasi kwa tukio lolote watakalofanyiwa wafuasi wao bila kuwa na hatia kwa kuwa kila wanapokaa kimya ndipo vitendo hivyo vinaongezeka huku wafuasi wao wakiteseka.

Aliwataka wafuasi wa CCM na viongozi wa chama hicho wasiwe na wasiwasi kwa kuwa CUF haitashiriki uchaguzi wa marudio na ushindi wataupata kwa kuwa vyama vinavyoshindana na CCM katika uchaguzi huo, havitafikisha hata asilimia moja ya kura.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Hamad Masoud Hamad, alisema viongozi wa nchi kutoka CCM ndio wanaoifikisha Zanzibar pabaya ili wananchi wasielewane kwa sababu ya itikadi za kisiasa.

Alisema kuwa kuna mambo mengi yameandaliwa katika uchaguzi wa marudiano utakaofanyika Machi 20, mwaka huu, ikiwamo kuwadhalilisha na kuwapiga wafuasi wa CUF, hasa kisiwani Pemba.

“Kipindi hiki Zanzibar ni tete. Tulitegemea kila mtu atakuwa na hamu ya kuja Zanzibar na kuishi lakini siyo kabisa na tulivyotarajia. Imefika mahali sasa watu wanapigwa,” alisema Hamad.

Habari Kubwa