CWT yageukia kilio nyumba za walimu

08May 2022
Augusta Njoji
Nipashe Jumapili
CWT yageukia kilio nyumba za walimu

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimetaja mambo sita yaliyotekelezwa kwa walimu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan huku kikiomba mkazo zaidi kwenye ujenzi wa nyumba za walimu hususan maeneo ya vijijini.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Kaimu Rais wa CWT, Dinnah Mathamani, alisema uhaba wa nyumba za walimu ni tatizo kubwa hasa vijijini.

 

“Walimu wanaoajiriwa wengi watakwenda vijijini ambako kuna uhaba wa walimu, zaidi kuliko mijini, lakini kule wanakokwenda nyumba za kupanga hakuna, watu wanaishi tu kijamaa, kuna nyumba ya mwenyekiti au mratibu.

 

“Kuna wakati walimu wetu wanapokewa kwenye jamii ile wanaishi katika familia kadhaa bila kuwapo na nyumba ambayo walimu wanaweza kuishi kwa amani na kuandaa masomo, lakini mtu anahitaji kuwa na 'privacy' (faragha) yake,” alisema.

 

Alieleza kuwa serikali katika bajeti yake ya 2022/23 imetenga Sh. bilioni 55.57 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 809 ambazo zitakaliwa na kaya 1,916 za walimu na kuomba bajeti iongezwe kutokana na kuwa na uhaba mkubwa.

 

“Kupanga bajeti na kuitamka ni jambo la kwanza lakini utekelezaji ni jambo lingine, sisi Chama cha Walimu tunaomba serikali yetu kwa nia hiyo njema ya kuweka bajeti, kuona umuhimu wa walimu na kuwajengea mazingira mazuri, ikasimamie hilo na hizo fedha zitumike kwa ajili ya kuwajengea walimu nyumba ili kuishi mazingira mazuri na kufundisha wanafunzi vizuri,” alisema.

 

Akizungumzia mambo sita yaliyotekelezwa na Rais, kiongozi huyo alisema serikali imeendelea kutekeleza mambo mbalimbali kulingana na mahitaji ya walimu ikiwamo upandishaji wa madaraja ambapo kwa mwaka 2021/22 walimu 127,000 walipandishwa madaraja huku wengine 52,000 wakitarajia kupandishwa mwaka huu.

 

Pia alisema serikali imeajiri walimu na hivyo kupunguza uhaba mkubwa wa walimu uliokuwapo ambapo kuna baadhi ya shule walimu walikuwa wakibeba mzigo mkubwa wa vipindi darasani.

 

“Kuna maeneo vijijini walimu wapo watano au sita na hata wanne na malengo ni yale yale wanafunzi wafaulu kwa kiwango kinachotakiwa, ilikuwa ni wakati mgumu kwa walimu lakini bahati nzuri kilio kimesikika, serikali imekuwa ikiongeza walimu kwa awamu ambapo awamu ya kwanza 13,000, ya pili 7,000, ya tatu 6,000 kwa mwaka 2020/21.

 

“Walimu walikuwa na mzigo mkubwa, walikuwa wanafundisha vipindi 35 hadi 40, kuongezeka kwa walimu watakwenda kuwapunguzia mzigo wa vipindi kwa walimu na kuwapa fursa ya kujiandaa vizuri kufundisha,” alisema.

 

Kadhalika, alimshukuru Rais kwa kusikia kilio chao cha kuwapatia stahiki zao waliokumbwa na vyeti feki lakini na wale wa darasa la saba waliokuwa wamefika muda wa kustaafu.

 

Alisema kwa mwaka 2021 pamoja na janga la UVIKO-19, kupanda kwa mafuta, vita vya Ukraine na Russia, Rais aliweka nguvu kazi na ujenzi wa madarasa 15,000.

 

“Tunalipongeza kwa kufanya hili kwa ajili ya Watanzania na wanafunzi, walimu sasa wanafundisha kwa nafasi sasa, zamani mwalimu alikuwa akifundisha wanafunzi wamejazana hadi karibu na ubao, na sasa hakuna msongamano kwenye madarasa,” alisifu.

 

Kuhusu madeni mbalimbali, Kaimu Rais huyo alisema serikali imeendelea kulipa siku hadi siku kwa madeni yaliyohakikiwa na kuomba yaliyopo yahakikiwe na yalipwe kwa wakati ili walimu wawe na utulivu shuleni badala kushinda kwenye ofisi za wakurugenzi wa halmashauri kufuatilia madai.

 

“Walimu tunamshukuru Rais Samia kutokana na kuona kwa muda mrefu mishahara haijapandishwa na amesema jambo letu lipo pale pale, tunasubiri hilo la mishahara kwa hamu kwa kuwa lipo hatua ya mwisho ya utekelezaji,” alisema.

 

Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif, alisema kutokana na yanayofanywa na serikali, ni wajibu wao walimu sasa kufundisha ipasavyo.

Habari Kubwa