Dada wa kazi atuhumiwa kunyonga mtoto wa bosi

31Jan 2021
Halfani Chusi
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Dada wa kazi atuhumiwa kunyonga mtoto wa bosi

JESHI la Polisi linamsaka mfanyakazi wa ndani, ambaye utambulisho wake wa majina una utata, kwa tuhuma za kumuua mtoto wa bosi wake kwa kumnyonga.

Hidaya Ali, mkazi wa Kawe Mzimuni jijini Dara es Salaam ambaye ni mama wa mtoto anayedaiwa kuuawa kwa kunyongwa, alisema tukio hilo lilitokea Jumatano nyumbani kwake.

Alisema kuwa mtoto wake wa kike mwenye umri wa miezi 10, aliuawa kwa kunyongwa na mfanyakazi wake huyo kisha kutoweka nyumbani.

"Siku ambayo mwanangu alinyongwa na kufa, niliamka asubuhi na dada wa kazi tukaenda sokoni kununua vifaa vya nyumbani ili tupike kabisa chakula niwaache na chakula kabla sijaenda kazini.

"Mimi huwa ninaondoka saa tano mchana na kurudi saa tano usiku, lakini kwa bahati mbaya tulichelewa kurudi sokoni, hivyo nikashindwa kuwapikia chakula.

"Nikamuachia pesa ya matumizi mfanyakazi wangu ale kwa kuwa mtoto alikuwa amekunywa uji. Baada ya hapo, nikaondoka kuelekea kazini.

"Ilipofika saa mbili usiku, nikapiga simu nyumbani kuongea na dada wa kazi ili kujua wanaendeleaje na mwannagu akapokea simu huku nikisikia sauti ya mwanangu kwa mbali analia, nikamuuliza 'mbona mtoto analia?'

"Dada akanijibu 'anataka kulala ndiyo maana analia, siunajua huyu akitaka kulala, lazima alie kwanza', nikamwambia sawa mbembeleze alale.

"Basi tokea hapo sikumpigia tena simu mpaka muda wa kurudi. Wakati wa kurudi, nilipofika nyumbani nikakuta milango yote imerudishiwa na taa zimezimwa, nikaingia sebuleni nikakuta maziwa hayajafunikwa, sebuleni kupo ovyo ovyo.

"Kufungua mlango wa chumbani, ninakuta mwanangu Heleni Chistopher, damu na mapovu vinamtoka hadi vimekauka na yeye akionekana kakabwa shingoni hadi kufa.

"Nilipiga kelele kwa sababu tukio hilo niliona ni la ajabu, watu wakajaa akiwamo mjumbe wa serikali ya mtaa, tukaita polisi kutoka Kituo cha Kawe wakaja kuuchukua mwili na kuupeleka Hospitali ya Lugalo," alisimulia.

Mama huyo alidai kuwa dada huyo alimtoa Morogoro miezi miwili iliyopita, akijitambulisha kwa jina la Lillian na kudai ana umri wa miaka 19, lakini siku chache kabla ya kutokea kwa tukio hilo, alibaini dada huyo ana kitambulisho cha taifa chenye picha yake na jina la Jesca. 

Kamanda Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai, alipotafutwa na Nipashe jana, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

"Baada ya mwili kufika kituo cha polisi, tuliupeleka Hospital ya Lugalo ambako baada ya uchunguzi, daktari alitueleza kuwa mtoto ameuawa kwa kukabwa na kitu shingoni.

"Sasa, Jeshi la Polisi linaendelea na taratibu za kumtafuta mtuhumiwa popote alipo kwa sababu inaonekana baada ya kufanya tukio hilo, alikimbilia kusikojulikana," alisema.

Kamanda huyo alitoa wito kwa wafanyakazi wa ndani kutojichukulia sheria mkononi na badala yake wafike kwenye mamlaka husika kama kuna stahiki hawajatimiziwa.

Habari Kubwa