Daftari la wapiga kura lina wapigakura milioni 29

01Aug 2020
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Daftari la wapiga kura lina wapigakura milioni 29

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa mstaafu, Semistocles Kaijage, amesema daftari la wapiga kura lina  wapigakura milioni 29,188,347. 

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa mstaafu, Semistocles Kaijage.

Amesema hayo leo katika kikao baina ya NEC na vyama vya siasa nchini.

Amesema bajeti inayotarajiwa kutumika katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu ni Sh. Bilioni 331.7.

Amesema kutakuwa na vituo 80,155 vya kupigia kura na kila kimoja kitakuwa na wapiga kura wasiozidi 500.

Jaji wa Rufaa mstaafu Kaijage amesema jumla ya asasi za kiraia 97 zenye nia ya kuwa watazamaji wa uchaguzi ndizo zimekidhi vigezo na tayari zimepewa  taarifa na zinasubiri kupewa vibali wakati ukifika.

Amesema kwa upande wa watazamaji wa uchaguzi wa Kimataifa mwaliko umetolewa na mchakato wa kupokea maombi unaendelea."Wakati ukifika tutawajulisha idadi ya waombaji hao," amesema.

Kuhusu malalamiko ya baadhi ya watendaji wa uchaguzi kutokuwapo ofisini wakati wa uteuzi wa wagombea, Kaijage amesema kitendo hicho ni kinyume cha maadili na kwa namna yoyote hakikubaliki.

" Tume tayari imekutana na wasimamizi wote wa uchaguzi upande wa Tanzania Bara Julai24, jijini Dodoma na msisitizo uliotokewa wazingatie maadili ya Uchaguzi na maelekezo yanayotolewa na NEC,"

Amesema tayari wasimamizi wa uchaguzi wamekwisha kuteuliwa na wanaendelea na mafunzo ambayo yatakamilika Jumatatu.

Pia amevitaka vyama kuwasisitizia wagombea wahakikishe wanajaza fomu kwa usahihi ili kuepuka dosari zinazoweza kuwafanya kushindwa kushindwa kuteuliwa.

Amesema wagombea wana haki ya kisheria ya kuweka pingamizi dhidi ya mgombea mwenzake  na kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Vyama vya Siasa ni miongoni mwa waliopewa haki hiyo.

Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Charles, amesema katika kampeni za uchaguzi wagombea wanatakiwa kutumia lugha ya Kiswahili tu na kama eneo husika hawajui pawepo mkalimani.

Pia amesema haitaruhusiwa kampeni kwenye nyumba za ibada au kutumia viongozi wa dini kuwafanyia kampeni.

Habari Kubwa