Dakika 30 za upepo zakosesha 700 makazi

07Nov 2016
Rose Jacob
UKEREWE
Nipashe
Dakika 30 za upepo zakosesha 700 makazi

BAADA ya tetemeko la Septemba 10 lililoacha vifo vya watu 17 na uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu kwenye Kanda ya Ziwa, lakini hasa mkoani Kagera,

Kaya 118 zenye watu zaidi ya 700 katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, zimekosa makazi, baada ya nyumba zao kubomolewa na nyingine kuezuliwa na mvua iliyonyesha kwa dakika 30 ikiwa imeambatana na upepo mkali juzi.

Tetemeko hilo lilielezwa kuwa na ukubwa wa 5.7 katika vipimo vya majanga hayo kimataifa, na kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa earthquaketrack.com ndilo kubwa zaidi katika historia kutokea nchini katika miaka ya 2010.

Mvua hiyo ya juzi iliyoambatana na upepo mkali, ilinyesha usiku na kusababisha athari kadhaa, ikiwamo kuharibu mazao mashambani na watu watatu kujeruhiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Francis Chang’ah, akizungumza na waathirika wa tukio hilo, alisema Serikali imeguswa na hali hiyo na kutoa msaada wa mabati 200 na magodoro 20, vikiwa na thamani ya Sh. milioni nane.

Chang'ah alivitaja vijiji vilivyokumbwa na maafa hayo kuwa ni Chakamba, Igara, Bwasa na Lugara na kueleza kuwa mbali na nyumba za wananachi, pia baadhi ya nyumba za ibada zilibomolewa.

Alisema kutokana na halo hiyo, watu walioathiriwa na tukio hilo wanalala nje.

“Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ilishatutahadharisha mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwa itakuwa na mvua kubwa, hivyo ni lazima mchukue tahadhari mapema kuondokana na maafa haya,” alisema Chang’ah.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Frank Bahati aliwaomba wadau mbalimbali wa wilaya hiyo na nje ya mkoa huo kujitokeza kuwasaidia waathirika hao misaada inayohitajika ikiwamo ya chakula na vifaa vya ujenzi kama saruji na mabati.

“Sisi halmashauri tumeona tujikune pale tulipoweza, ukiangalia kuna nyumba za walimu mbili zimeezuliwa na kila nyumba tumetoa mabati 30 ili wazifanyie marekebisho ya haraka,” alisema Bahati.

Waathirika wa tukio hilo Malia Kamese na Masumbuko Bundala, walisema wanalala nje nje na wengine hawana chakula, hivyo wanaiomba Serikali kuongeza misaada.

“Tunaishukuru Serikali yetu ya wilaya kwa kutusaidia misaada hii, lakini tunaomba waendelee kuleta mingine zaidi kwa kuwa kuna wengine watakosa,” alisema Bundala.

Diwani wa Kata ya Igara, Joshua Manumbu, alisema licha ya misaada hiyo kuwa michache, lakini wataigawa kwa watu walioathirika lakini zaidi kwa wazee wakati wakiendelea kusubiri misaada mingine.

Habari Kubwa