Daktari feki anaswa akidaiwa kutoa huduma za kibingwa

29Apr 2021
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Daktari feki anaswa akidaiwa kutoa huduma za kibingwa

MKAZI wa Kijiji cha Mudio, Kata ya Romu wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Othuman Kimaro, amekamatwa na vyombo vya dola akituhumiwa kujifanya daktari na kutoa huduma za kitabibu kwa wagonjwa, zikiwamo zinazotakiwa kutolewa na madaktari bingwa.

MKAZI wa Kijiji cha Mudio, Kata ya Romu wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Othuman Kimaro.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, aliagiza kukamatwa na kuhojiwa kwa Othuman baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kuzuru kwenye zahanati bubu inayodaiwa kutumiwa na mtuhumiwa huyo kutibu wagonjwa, huku akiwa hana leseni ya kufanya kazi hiyo.

"Sasa hivi kuna mtoto yuko Hospitali ya Rufani ya KCMC amelazwa kule akipatiwa matibabu kwa sababu ya mambo haya. OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya), TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) na Ofisa Mtendaji wa Kata hii. Huyu mtu ninawaachia hapa.

"Ahojiwe na aeleze kwa nini anahatarisha uhai wa watu? Anaweza kugharimu maisha ya watu hapa Mudio na kwingineko kwa kutoa huduma za tiba wakati hata serikali haimtambui.

"Anatoa dawa, anaandika rekodi za wagonjwa na anafanya kazi nyingine zinazostahili kufanywa katika ngazi ya vituo vya afya na hospitali za wilaya.

"Ana lundo la dawa hatari ambazo hazitakiwi kutolewa nje ya hospitali au vituo vya afya, ana vifaa na dawa za kuosha kizazi. Maana yake anaweza kuwa ndiye kinara wa kufanya abortion (kutoa mimba)," Ole Sabaya aliagiza.

Alipoulizwa na kiongozi huyo kuhusu shughuli zinazoendelea kwenye nyumba aliyokutwa yenye dawa na duka la dawa, mtuhumiwa huyo alidai anatoa huduma za kifedha zinazotolewa kupitia miamala ya mitandao ya simu.

Akizungumza baada ya ukaguzi kufanyika katika zahanati bubu iliyoko Mudio, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Irine Haule, alisema:

"Leo Aprili 28 (jana), tumekuja na Mkuu wa Wilaya katika Kijiji cha Mudio, kuna mtu ambaye alikuwa analalamikiwa na wananchi kutoa huduma za afya kinyume cha utaratibu.

"Kimsingi, huyu mtu yeye mwenyewe anadai kwamba ni mtaalamu wa afya lakini amestaafu. Mpaka sasa sijafanikiwa kuona vyeti vyake vya afya. Pia tumekuta duka lenye dawa nyingi za kunywa pamoja na za kuchoma.

"Lakini kuna vifaa vingi ambavyo vinatumika katika hospitali na vifaa vya kutolea huduma. Vimo vifaa vya kusafisha vizazi, sindano pamoja na dripu.

"Kwa hiyo kimsingi anachokifanya ni kosa. Huyu bwana (Othuman), serikali haimtambui lakini pia taratibu anazozitumia kutolea huduma ni taratibu ambazo hazijafuata misingi ya miongozo ya wizara kama zilivyowekwa.

"Tumeona ana hizo dawa na sindano lakini mazingira ambayo anatolea huduma siyo sahihi. Ukiangalia katika matumizi yake ya dawa, anafanya kuandika kwenye makaratasi na kwenda kwenye maduka makuwa kununua."

Kutokana na upungufu huo, Dk. Haule aliwataka wenye maduka makubwa ya dawa kuchunguza mtu anayepaswa kwenda kununua dawa nyingi, hasa dawa hatari kwamba ni vyema mtoa huduma, akawa na uthibitisho kama anayenunua ana kibali cha kupata hizo dawa.