Daktari feki upasuaji anaswa

25Nov 2018
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe Jumapili
Daktari feki upasuaji anaswa

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia Hassan Athumani (38) mkazi wa kijiji cha Malimbika, Gairo mkoani Morogoro kwa tuhuma ya kujifanya daktari wa binadamu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, picha na mtandao

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake mjini hapa kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa akitoa huduma za kitabibu katika jengo lisilo rasmi ambalo linamilikiwa na Kisusa Iberi, mkazi wa kijiji cha Mwakisabe.

Alisema tukio hilo lilitokea Novemba 20, mwaka huu, majira ya 6:30 mchana katika kijiji hicho kilichoko wilayani Chemba mkoani hapa na kwamba wakati akikamatwa, walikutwa watu 14 wakipatiwa matibabu, mmoja kati ya hao akisubiri kufanyiwa upasuaji wa uvimbe ulioko katika paji la uso.

"Katika upekuzi tulio ufanya mtuhumiwa alikuwa na vitu mbalimbali kama vile dawa za ‘antibiotic’, dawa za maumivu, dawa za ganzi, sindano na dripu za maji, vifaa vingine vya tiba ambayo ni mashine ya BP (kupima shinikizo la damu), mashine ya kupimia kisukari na baadhi ya vifaa vya upasuaji," alisema Kamanda Muroto.

Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha mtuhumiwa huyo amewahi kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu mwaka 2015 katika mahakama ya wilaya ya Kongwa kwa kosa la kujifanya daktari wa binadamu lakini alitoroka akiwa kwenye dhamana.

Kamanda Muroto alisema mtuhumiwa huyo alikuwa bado anatafutwa ili akatumikie adhabu yake.

Katika hatua nyingine, Jeshi polisi Mkoani hapa limemkamata Mario Andrea (28) mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma kwa tuhuma za unyang'anyi wa kutumia silaha.

Kamanda Muroto alisema tukio hilo lilitokea Novemba juzi majira ya saa 1:00 usiku katika eneo la Nkuhungu.

"Mtuhumiwa huyo alikwenda kwenye kituo cha bodaboda akitaka impeleke nyumbani kwake na walipofika sehemu ambayo ina vichaka alimtaka mwendesha bodaboda asimame kidogo ndipo alipomtolea kisu na kumpora pikipiki yake yenye namba MC 865 AWAP aina ya Fekon, yenye rangi nyekundu," alisema Muroto.

Hata hivyo kamanda Muroto alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Habari Kubwa