Dalili moshi wa kijani U-spika CCM kuanza kuonekana rasmi

20Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Dalili moshi wa kijani U-spika CCM kuanza kuonekana rasmi

JOTO la uchaguzi wa spika ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) linazidi kupanda kutokana na kitendawili cha wanachama watatu kati ya 71 waliojitokeza kuomba nafasi hiyo kufanyika leo.

Awali kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kilipangwa kufanyika juzi, lakini kikasogezwa hadi leo. Kamati Kuu inatarajiwa kutoa majina matatu ya wanachama watakaopigiwa kura na wabunge wa chama hicho, kumrithi Job Ndugai, aliyejiuzulu hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, kikao hicho kitafanyika Makao Makuu ya CCM, Dodoma.

“Kikao hicho kitatanguliwa na kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Maandalizi ya vikao vyote hivyo yamekamilika,” alisema Shaka.

Kwa mujibu wa ratiba ya awali, uchukuaji fomu ulimalizika Januari 15, ukafuatiwa na kikao cha Sekretarieti Januari 17 na sasa ilisubiriwa kikao cha Kamati Kuu.

Baadhi ya makada waliojitokeza ni Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, aliyekuwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, aliyekuwa Waziri na Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba.

Wengine ni aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Bunge la Afrika (PAP) na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele na msomi aliyejinasibu ana shahada tisa, Baraka Byabato na Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku maarufu kama Msukuma.

Habari Kubwa