Dangote kuathiri ajira za maelfu

29Nov 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Dangote kuathiri ajira za maelfu

WADAU wa uchumi wamesema matokeo kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara kusitisha uzalishaji kutokana na kuelemewa na gharama za uendeshaji, ni kupukutika kwa maelfu ya ajira kuanzia wafanyakazi mpaka mama lishe.

Kwa mujibu wa tovuti ya serikali ya mkoa wa Mtwara, "kiwanda hiki ni kikubwa kuliko vyote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati" na kina uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu za saruji kwa mwaka.

Kilianza uzalishaji Septemba mwaka jana, baada ya uwekezaji wa dola za Marekani milioni 500 (sawa na Sh. trilioni 1.1).

Mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Joel Silas alisema kuwa hatua ya kiwanda hicho itasababisha upotevu wa ajira kwa wafanyakazi na mapato ya serikali katika kodi mbalimbali.

Alisema kama kiwanda, Dangote ilikuwa ikilipa kodi mbalimbali, lakini hata wafanyakazi na kiwanda walilipa kodi, ikiwemo PAYE, ambazo ziliingia serikalini moja kwa moja.

"Sasa (ajira) zinapositishwa," alisema Dk. Silas, "tafsiri ya haraka hakuna fedha itakayoingia serikalini."

“Athari nyingine ni kupungua kwa shughuli za kiuchumi ambazo zinatokana na uwepo wa kiwanda (cha Dangote katika mkoa wa Mtwara), hoteli, maduka na bar ambazo zilifunguliwa kwa sababu ya kiwanda."

Mchumi huyo alisema athari za kusitishwa uzalishaji katika kiwanda hicho zitajitokeza kwa wajasiriamali wadogo wanaochuuza kwa madereva na malori ya usafirishaji, wakiwemo mama lishe, kuanzia jirani na kilipo kiwanda mpaka mikoa ya mbali ambako saruji hiyo ilipelekwa.

"Mabenki ambayo yalifungua matawi kwa ajili ya kufanya kazi," alisema zaidi Dk. Silas. "Ina maana itabidi yasitishe huduma zao kwa vile hakuna shughuli za uzalishaji.”

Alitaja athari nyingine kuwa ni kusimama kwa upanuzi wa miundombinu kama ujenzi wa reli, bandari kwa ajili ya kusafirisha saruji ya Dangote nje ya nchi.

Dk. Silas alisema kwa ujumla pato la taifa litaathirika kwa kukosa mchango wa kiwanda hicho.

Aidha, msomi huyo alionyesha wasiwasi wake kwenye kufanikiwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano ulioweka mkazo katika viwanda.

Alisema kufungwa kwa kiwanda hicho kunatoa taswira mbaya kwa wawekezaji wengine wa kigeni, hivyo ni vyema serikali ikachukua hatua madhubuti kumaliza tofauti zilizopo kabla athari hazijawa kubwa.

Tayari Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameshatuma timu ya wataalamu kwenda kiwandani huko kwa mazungumzo na Dangote, hata hivyo.

“Kuondoa ubishi nimemwagiza Katibu Mkuu (Nishati), wenye makaa ya mawe Tancoal na Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC), waende kiwandani wazungumze nao,” Prof. Muhongo alisema jana.

Waziri huyo alisisitiza, hata hivyo, kuwa ni lazima malighafi ya nchini itumike kwa kuwa mwekezaji hawezi kuagiza nje huku akiacha iliyopo.

Alisema kukiwa na uhuru huo, kutakwamisha jitihada za serikali kuwa na viwanda vitakavyotumia malighafi ya nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Harpreet Duggal, aliiambia Nipashe kwa njia ya simu jana kuwa leo watatoa taarifa rasmi kuhusu kusimamisha uzalishaji huko, lakini mwishoni mwa wiki alisema pamoja na mengine, umetokana na gharama kubwa ambazo zimekuwa zikiwakabili katika kukiendesha.

Mwezi uliopita Mkurugenzi huyo alilalamikia uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku kiwanda chake kuingiza makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini na kutakiwa kutumia ya Liganga ambayo alidai ni ya chini ya kiwango na yanauzwa kwa bei ghali.

Duggal alililalamikia pia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa kushindwa kuwauzia gesi kwa bei rahisi, wakati inazalishwa mkoani Mtwara kilipo kiwanda chake.

Kushindwa kupatikana kwa nishati hizo mbili, alisema Duggal kumefanya Dangote kutumia lita 200,000 za mafuta ya diseli kwa siku, licha ya ahadi ya serikali wakati wa uwekezaji kuwa kingepata nishati ya umeme kwa bei rahisi.

Kiwanda hicho ambacho pia ni kikubwa zaidi Afrika Mashariki, kilianza uzalishaji mwaka mmoja uliopita na kimesaidia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo nchini.

DIPLOMASIA IKATUMIKA
Naye Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo cha Diplomasia, Dk. Wetengere Kitojo, alisema Dangote ni mzalishaji mkubwa wa saruji ambaye alisaidia kupungua kwa bei kutoka wastani wa Sh. 15,000 hadi 12,000 na uwepo wa saruji ya kutosha.

Alibainisha kuwa athari zitakazojitokeza ni kupanda kwa bei ya saruji, kutikisika kwa azma ya serikali ya wananchi wake kuwa na makazi bora, kuongezeka kwa gharama za ujenzi ambazo zitaathiri gharama za kodi.

Alisema ni vyema diplomasia ikatumika kumaliza tofauti zilizopo ili kuwa na suluhisho katika kuepusha athari kwa wananchi, mwekezaji na wananchi kwa ujumla.

“Wawekezaji wengine wenye nia wakiona huyu anasuguana na serikali wanaweza kusita kuja kuwekeza," alisema Dk. Kitojo.
"Ni vyema wakae wayamalize kuliko kuchafua hali ya hewa nchini.”

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Kapuulya Musomba, alisema mwishoni mwa mwezi uliopita kuwa shirika lake linauza gesi kwa sheria na taratibu zilizopo na kwamba bei elekezi inapangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura).

Alisema hayo wakati akijibu malalamiko ya Duggal kuwa TPDC inataka kuwauzia gesi kwa bei ya wateja wa Dar es Salaam ilhali kiwanda hicho kipo inapotoka gesi yenyewe.

Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema TPDC inadanganya inaposema kuwa wao ndiyo wanapanga bei.

Alisema bei nyingine inapangwa na TPDC, na kwamba kuanzia mwakani bila kujali kama kampuni hiyo imewasilisha maombi au la, wakala wake itaanza kupanga bei inayoendana na umbali na kwamba kila baada ya kilomita 100 kutakuwa na bei yake.

“Kila mtumiaji wa gesi atakuwa na bei yake," alisema Kaguo.

"Wapo wa viwanda vikubwa, vya mbolea, umeme, gesi ya kwenye magari na majumbani, kila mmoja atakuwa na bei yake.”

Aidha alisema TPDC ilitakiwa kuwa imewasilisha maombi tangu Jumatatu iliyopita ili kuruhusu kuanza kwa mchakato wa kutoa bei elekezi, lakini hadi sasa hajawasilisha maombi hayo.

Alisema Ewura hawana jukumu la kupanga bei ya gesi yote bali ya kuchakata, kusafirisha na kusambaza na kwamba kuna bei nyingine za TPDC na wadau wangine.

Habari Kubwa