Dangote wapanda miti 1,000 kuunga mkono ahadi ya Samia UN

27Sep 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe
Dangote wapanda miti 1,000 kuunga mkono ahadi ya Samia UN

WAFANYAKAZI wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote cha mkoani Mtwara wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kiwanda hicho,Amadurai Appavoo,pamoja na wakazi wa Halmashauri hiyo wamepanda jumla ya miti 1,000 kiwandani hapo na eneo jirani.

Akizungumza mara baada ya upandaji wa miti hiyo,Meneja Mawasilano wa Dangote, Recho Singo, amesema upandaji huo wa miti unaenda sambamba na maadhimisho ya uzinduzi wa wiki ya malengo endelevu ya umoja wa Mataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hivi karibuni Rais  Samia alipozungumza katika mkutano wa viongozi wakuu wa nchi katika mkutano wa umoja wa mataifa aliahidi Tanzania kuipa kipaumbele utunzaji wa mazingira, jukumu linalopaswa kufanywa na kila mwananchi kwa ajili ya kuunga mkono ahadi hiyo ya Rais kwa ulimwengu.

"Mbali na kupanda miti hii katika eneo linalozunguka kiwanda chetu cha Dangote hususan katika eneo la chanzo cha  uhifadhi w maji lakini pia tumepanda miti mingine katika kijiji cha Mbuo na eneo la Shule ya Msingi ya Dunstan Kyobya iliyopo katika kijiji cha Hiari."amesema Singo.

Amesema upandaji miti huo katika maeneo mbali mbali ya Mtwara itakuwa ni suala endelevu lkwa ajili ya  kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania katika kulinda na kuhifadhi mazingira, na kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa ajili ya kukabiliana na changmoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Dangote kama Taasisi duniani kote wiki hii ni muhimu sana kwetu, tunaungana na Umoja wa Mataifa kutekeleza malengo endelevu 17 ambapo kitaifa sisi Dangote Tanzania tunatekeleza malengo matatu ambapo moja wapo ni kutatua changmoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi,” amesema.

Amesema Watanzania wengi wamekuwa na tabia ya kukata miti pasipo kupanda mbadala wake hali inayosababisha  kuwepo kwa athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia  nchi ambayo huathiri mazingira na maisha ya watu, ikiwa ni pamoja na kukosa hewa safi.

Ameongeza kuwa ni vema uhamasishaji ufanyike zaidi juu ya upandaji miti ili atakayekata mti mmoja awajibike  kupanda miti angalau mitano.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuo, Andullah Mohamed ameushukuru uongozi wa Kiwanda hicho kwa kupanda miti katika kijiji chake na kusema miti hiyo itasaidia katika kulinda mazingira na chanzo cha maji kilichopo katika eneo la kijiji.

“Kwanza ninashukuru Dangote kwa zoezi hili la upandaji miti maeneo ya kijiji changu hii itatusaidia kuhifadhi vyanzo vyetu vya maji ili visiweze kukauka, vyanzo vya maji vikikauka ni hasara kwa jamii nzima, na kwa bahati nzuri vyanzo hivi vinanywesha vijiji visivyopungua kumi na nne Mtwara DC,”amesema Mohamed