Dar kinara ukatili wa wanawake

25Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Dar kinara ukatili wa wanawake

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, ametaja mikoa mitano yenye kiwango cha juu cha ukatili wa wanawake kwa mwaka 2019/20, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam matukio yaliyoripotiwa ni 2,618, ukifuatiwa na Arusha (1,393), Tanga (1,352), Lindi (1,161) na Manyara (968).

Kufuatia hali hiyo, ameagiza wataalamu wa maendeleo ya jamii kusaidia mikoa hiyo kubaini tatizo la kuongoza kwa vitendo hivyo licha ya kuwa na maendeleo makubwa.

Dk. Gwajima aliyasema hayo, jana, alipokuwa akifungua Kongamano la Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA), jijini hapa.

“Eti mikoa iliyoongoza ushangae wewe wanasema maendeleo ni makubwa wanaendeleza na matukio ya ukatili…Tatizo nini kwenye hii miji yetu mikubwa yenye TV kila nyumba, wasomi na barabara zipo mjini, twendeni tukawasaidie tatizo ni nini?” Alihoji.

Alisema takwimu hizo sio nzuri na haipendezi na inahitaji kuimarisha nguvu kubwa ya kuzungumza na jamii kwa kutumia taaluma yao.

“Tunataka katika miaka ijayo hii hali ishuke, serikali itaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ukatili, hizi kamati za MTAKUWWA hakikisheni zinasimamia na kutokomeza ukatili wa wanawake na watoto kwenye maeneo yao,” alisema.

Alisema katika kipindi hicho cha mwaka 2019/20 matukio ya ukatili dhidi ya watoto 14,891 yameripotiwa katika mikoa mbalimbali.

Hata hivyo, alisema kuna maofisa maendeleo ya jamii wengine bado hawajaunda kamati hizo na kuagiza kupatiwa taarifa ili kuwahoji ambao hawajafanya vizuri.

Kadhalika, aliagiza kupatiwa taarifa ya halmashauri ambazo hazifanyi vizuri kwenye utoaji wa mikopo kwa wanawake licha ya serikali kutenga fedha hizo.

“Kwenye baadhi ya maeneo bado kuna shida, wananchi bado hawaelewi uwapo wa fursa za mikopo, naomba niagize Katibu Mkuu nipate taarifa katika halmashauri zetu zote zipi zinafanya vizuri na kufikia kutumia fedha asilimia 100 na zipi zipo chini, niende huko wakanieleze,” alisema.

Aliongeza, “Tunataka tujue hela ya serikali imetolewa, je, umehamasishaje hawa watu? Simama mwana maendeleo ya jamii, nenda kwenye mtaa waeleze fursa kwamba serikali yao inatoa fedha zinatumika hadi kuisha na si kubaki.”

Aidha, alisema serikali inatekeleza Mpango wa Miaka Mitano (2017/18 – 2021/22) wa kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za kujitegemea na kujiletea maendeleo.

“Mpango huu ni muhimu kwa kuwa unatoa mwongozo na mwelekeo kwa wadau na wataalamu wa maendeleo ya jamii katika kuhamasisha jamii iweze kujitolea katika shughuli za kujitegemea na serikali kupitia mpango huu inatekeleza kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha jamii kuboresha makazi kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla,” alisema.

Naye Rais wa CODEPATA, Sunday Wambura, alisema wapo tayari wataalamu hao kutekeleza maelekezo ya waziri ikiwamo matukio ya ukatili.

 

Habari Kubwa