Dar kuwa na joto kali hadi mwakani

09Dec 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Dar kuwa na joto kali hadi mwakani

MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA), imezungumzia hali ya joto iliyopo mikoa ya pwani na Dar es Salaam na kusema joto kali zaidi linakuja sasa hadi mwakani.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri TMA, Samwel Mbuya, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa unaotolewa kila siku na TMA.

Mbuya alisema mwezi huu joto limekuwa juu ya wastani hadi nyuzi joto 35 katika maeneo ya  mkoa wa Pwani huku Dar es Salaam kukiwa na nyuzi joto 34.

“Joto hili litaendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu na tunatarajia Januari litapungua lakini Februari 2019 jua la utosi litajitokeza tena na kwa sababu si kipindi cha mvua joto litakuwa kali zaidi ya hili la sasa,” alisema.

Taarifa ilisema mwezi huu wakulima wasitarajie kuwa na mvua nyingi, ingawa zitakuwa za wastani hadi chini ya wastani.

“Kinachosababisha joto hili ni mwenendo wa kawaida wa mifumo ya hali ya hewa ambayo katika eneo la kusini mwa mstari wa Ikweta, kipindi hiki kunakuwa na jua la utosi ambalo kwetu Tanzania inakuwa miezi ya Novemba mwishoni na Desemba,” alisema.

Alisema ndiyo maana kumekuwa na ongezeko la vipindi vya joto hususan ukanda wa pwani na katika msimu huu wa mvua za vuli maeneo hayo mtawanyiko wa mvua ni hafifu.

“Kwa hiyo, hali ya joto, fukuto huongezeka zaidi ukanda wa Pwani kuliko maeneo mengine ambayo yanapata msimu wa vuli na mvua za msimu,” alisema.

Aidha, Mbuya alisema kuwepo kwa jua la utosi na hali ya mtawanyiko hafifu wa mvua za vuli kumesababisha ongezeko la joto na fukuto katika maeneo hayo.

“Baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini, Mashariki, hali ya mtawanyiko wa mvua za vuli siyo ya kuridhisha,” alisema.

Alisema viwango vya joto bado vipo katika wastani, hivyo kuleta hali ya joto kali na fukuto linalotokana na ongezeko la unyevu unyevu katika kipindi hiki cha msimu,” alisema.

Akieleza kitaalam zaidi, Mbuya alisema kwa kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila mwaka, jua la utosi huwa katika maeneo ya kizio cha Kusini mwa dunia.

 

Tanzania ikiwa moja ya nchi zilizoko katika kizio cha kusini huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi wakati huu  ikilinganishwa na miezi mingine.

 

Vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele kati ya mwishoni mwa mwezi Novemba na Disemba wakati linaelekea kusini kwenye Tropiki ya Kaprikoni na hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likielekea kaskazini kweye Tropiki ya Kansa, alisema.

Habari Kubwa