Dawa waathirika wa ‘kubeti’ yaja

14Nov 2019
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Dawa waathirika wa ‘kubeti’ yaja

SERIKALI imesema inaandaa utaratibu wa kuanza kutoa tiba kwa Watanzania ambao wamepata uraibu kutokana na kujihusisha kupita kiasi na michezo ya kubahatisha, maarufu kama kubeti.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, picha mtandao

Pia imesema imeshaanza kuchukua hatua ya kujenga mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) utakaotumika katika kusimamia mapato yatokanayo na michezo hiyo pamoja na kuratibu mienendo ya wachezaji kwa nia ya kukabiliana na uraibu wa michezo hiyo.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Ileje (CCM), Janet Mbene, aliyetaka kujua athari zitokanazo na michezo ya kubahatisha.

Mbene pia alitaka kujua mipango ya serikali katika kuchukua tahadhari za kuhakikisha michezo ya kubahatisha inashirikisha watu wenye ufahamu wa athari za kutegemea michezo hiyo, hali inayoweza kuwaletea athari kubwa za kiuchumi, kijamii hadi ndani ya familia na taifa.

Dk. Kijaji alisema: "Serikali inaandaa utaratibu wa kuanza kutoa tiba kwa wachezaji ambao wamepata uraibu kutokana na kujihusisha kupita kiasi kwenye michezo ya kubahatisha."

Aliongeza kuwa serikali imeshaanza kutoa elimu kwa umma kuhusu athari hasi zitokanazo na michezo ya kubahatisha, kudhibiti uagizaji na uendeshaji holela wa michezo hiyo hususani ya mitandaoni.

Pia alisema serikali nimeshaanza kuboresha sheria ya michezo ya kubahatisha kwa lengo la kukabiliana na athari za michezo hiyo.

Dk. Kijaji alisema athari zilizochukuliwa na serikali zinalenga kupunguza ushawishi wa kushiriki michezo ya kubahatisha kupita kiasi na hivyo kupunguza athari hasi zitokanazo na michezo ya kubahatisha kwa jamii.

Alisema hivi sasa kuna changamoto ya kusimamia wachezaji wa michezo ya kubahatisha, hususani wachezaji wa michezo isiyohusisha mfumo wa Tehama.

Kwa mujibu wa Kijaji, serikali iko mbioni kuunganisha michezo yote kwenye mfumo huo unaoendelea kujengwa, utaanza kutumika Januari, mwakani.

"Mfumo huu utaiwezesha serikali kuratibu mienendo ya kila mchezaji na kuchukua hatua dhidi ya wale wanaokiuka sheria na kanuni za michezo ya kubahatisha. Mfumo huo utatumika pia kudhibiti uchezaji uliokithiri kwa kuweka viwango vya fedha za kuchezwa," alisema Dk. Kijaji.

Alisema kwa michezo inayoendeshwa kwa mfumo wa kompyuta, usimamizi wa wachezaji unafanyika kwa kuwa taarifa za mchezaji huchukuliwa kikamilifu na hivyo serikali inaweza kuwatambua na kuwasimamia kupitia taarifa zao.

"Pale inapobainika kuwa mchezaji ameathirika kutokana na kujihusisha kwenye michezo ya kubahatisha (kucheza kupita kiasi), hufungiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GMT) kwa kushirikiana na waendeshaji," alisema Dk. Kijaji.

Naye Mbunge wa Geita Vijiji (CCM), Joseph Kasheku ‘Musukuma’, aliomba mwongozo bungeni akitaka apewe majibu kuhusiana na michezo ya kubahatisha kuchezwa na wanafunzi na watoto katika maeneo ya vijijini.

Musukuma alidai kwamba mashine za kamari zilizopo katika maeneo ya vijijini watoto na wanafunzi wamekuwa wakicheza huku wahusika wakiwa wanaangalia tu.

"Mashine za kamari zilizopo huko vijijini kwetu zimetuletea tabu sana hasa kwa wanafunzi, zimewekwa hovyo tu mtaani wanacheza kuanzia asubuhi mpaka jioni, nilitaka nipewe utaratibu huu unaotumiwa na Wachina vijiji kwetu upo halali?,"alihoji Musukuma.

Akitoa majibu ya serikali, Dk. Kijaji alisema michezo ya kubahatisha inaendeshwa kulingana na sheria ya michezo ya kubahatisha ya mwaka 2003 pamoja na marekebisho yake yaliyofanyika mwaka 2019.

Habari Kubwa