DAWASA watekeleza agizo la Magufuli,maji kufika Ukonga,Segerea

23Dec 2020
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
DAWASA watekeleza agizo la Magufuli,maji kufika Ukonga,Segerea

Kufuatia agizo la Rais Dk. John Magufuli la kutaka Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kufikisha huduma ya Maji safi kwa wakazi wa Pugu, Gongo la Mboto, Majohe, Chanika,Ukonga na Segerea kabla ya Desemba 25 Mwaka huu, limetekelezwa.

Akizungumza wakati wa kukagua maendeleo ya ukamilishaji wa mradi huo leo Desemba 23,2020, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amejionea ukamilishaji wa Mradi wa Ujenzi wa Tangi kubwa la Maji linalopokea maji kutoka Kisarawe kwenda Pugu lenye uwezo wa kupokea na kusambaza Lita Milioni 2.8 kwa siku lililojengwa kwa thamani ya shilingi Bilioni 6.9 lililoanza kupokea maji na kuyasambaza kwa wananchi.

Mradi huo utahudumia wakazi wa Jimbo la Ukonga ikiwemo Pugu, Majohe, Gongo la Mboto, Bangulo, Airwing, Kigogo, Chanika, Kinyamwezi, Banana, Segerea na Kifuru.

Aweso ameonyesha kufurahishwa na utekelezaji wa agizo hilo ndani ya muda mfupi na kuwataka DAWASA kuwekeza nguvu zaidi katika kuwaunganishia wananchi huduma hiyo ili kila mwananchi awe na huduma.

"Mradi huu tumeutekeleza Wizara kupitia DAWASA na ni faraja kwetu kuwa umekamilika ndani ya wakati na unaenda kuondoa shida yote ya Maji kwa   maeneo yaliyopitiwa na mabomba hayo kuanzia Pugu hadi Kinyerezi"amesema  Aweso

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge ametoa wito kwa wananchi kulipa bili za Maji ili kuiwezesha DAWASA kuendelea kupanua huduma kwani miradi mingi inayofanywa na Mamlaka hiyo inatumia fedha zake za ndani zitokananazo na makusanyo ya ankara za huduma ya Maji.

Aidha RC Kunenge amesema Serikali itawachukulia hatua za kisheria wezi wa maji na wanaoharibu miundombinu ya Maji huku akiwaelekeza DAWASA kudhibiti tatizo la upotevu wa Maji.

Mradi wa Maji Kisarawe-Pugu - Gongo la mboto umetekelezwa na DAWASA baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji Kibamba- Kisarawe ulioleta uhitaji kwa wananchi wa maeneo hayo.  Jumla ya shilingi Bilioni 6.9 zimetumika hadi kukamilisha kwa mradi huo utakaonufaisha wakazi takribani 450,000. 

Habari Kubwa