Dawasa yakabidhiwa mradi wa Same-Mwanga-Korogwe

20Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
KILIMANJARO
Nipashe
Dawasa yakabidhiwa mradi wa Same-Mwanga-Korogwe

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam(DAWASA) imepewa kazi ya kukamilisha mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe baada ya wakandarasi wa awali kampuni za M.A Kharafi & Sons na BADR East African Enterprises Ltd kusuasua katika utekelezaji mradi na kusitishiwa mkataba Desemba 2020.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akikata utepe kuashiria uzinduzi wa uendelezaji wa ujenzi wa Mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiongea katika hafla fupi ya makabidhiano ya mradi huo iliyofanyika jana wilayani Mwanga amesema Serikali itasimamia haki na madai ya malipo ya wafanyakazi waliofanya kazi na kampuni hizo, na haitamvumilia mkandarasi mzembe au mtaalam atakayechelewesha mradi wa maji kukamilika kwa wakati.

 

Aweso alisema baadhi ya kazi kama ufungaji wa mifumo na mitambo ya umeme (electro mechanical) zitafanywa na wakandarasi na utaratibu wa kuwapata umeshaanza ili kila jambo lifanyike kwa wakati na kukamilika. Aidha, Waziri amewataka wataalam wa manunuzi kuhakikisha watoa huduma na wakandarasi wanaopatikana wanakuwa bora ili kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kama ilvyopangwa.

Meza kuu wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe kwa DUWASA.

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi, Anthony Sanga akiongea katika hafla hiyo amesema Serikali na wataalam wake wamejipanga kuchukua miradi yote ambayo wakandarasi watalegalega katika kuzingatia mikataba ya kazi. Pamoja na hilo, ametoa onyo kwa wakandarasi wanaozidisha gharama za miradi kwa sababu watapoteza sifa za kutekeleza miradi hiyo.

 

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi. Cyprian Luhemeja amewahakikishia viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa kazi ya kukamilisha mradi huo wanaimudu, na kuahidi kazi itakamilishwa ifikapo Desemba 19, 2021.

 

Mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe utakaozalisha zaidi ya lita milioni 65 kwa siku utakuwa na tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni tisa ambalo litakuwa kubwa kuliko yote mkoani Kilimanjaro, na utahusisha ulazaji wa mabomba yenye urefu wa jumla ya kilomita 265. Mradi utafikisha kiwango cha upatikanaji huduma ya maji kwa asilimia 100 katika maeneo husika.

Habari Kubwa