DAWASA yapeleka maji Saranga, Mkuu wa wilaya Ubungo azindua

22Mar 2019
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
DAWASA yapeleka maji Saranga, Mkuu wa wilaya Ubungo azindua

Katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare  Makori amezindua mradi wa maji katika Kata ya Saranga utakao hudumia zaidi ya wakazi 15,000 wa Kata hiyo ambao walikuwa hawapati huduma ya majisafi tangu kuanzishwa kwa eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare  Makori, akizindua mradi wa maji katika kata ya saranga leo machi 22, 2019.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliokwenda sambsamba na maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani ambayo kitaifa yamehitimishwa leo Machi 22,2019 mkoani Dodoma, Makori amewaambia wakazi hao kuwa kukamilika kwa mradi huo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali  ya kuhakikisha inasogeza karibu huduma muhimu kwa wananchi. 

"Tangu maeneo haya yalipoundwa na kupewa jina la Saranga hakukuwahi kupata huduma ya Majisafi hizi zote ni juhudu za Rais John Magufuli za kuhakikisha huduma muhimu kama hizi zinafika karibu kwa wanachi na kuondokana na kero za upatikanaji wa maji na pia Waziri wa maji amewahi kufika hapa na aliahidi kuwa maji yatapatikana kilichofanyika ni utekelezaji tu wa kumtua mama ndoo kichwani," amesema Makori 

Amesema kuwa hii sio Serikali ya maneno, bali ni serikali ya vitendo ambayo inatekeleza Ilani ya CCM ambayo kwenye uchaguzi Rais Magufuli aliahidi kumtua mama ndoo ya maji kichwani kwa kumsogezea huduma ya maji karibu.

 Makori, amempongeza diwani wa kata ya Sranga kwa kushirikiana kwa karibu na DAWASA kufanikisha mradi huo unakamilika kwa wakati "Sisi tunazunguka na kufanya maendeleo nyie achaneni na wanaozunguka na kutetea ushoga nadhani mnamjua nikisema hivyo" amesema Makori

"Leo tunaenda kuzindua kizimba cha Maji niwaombe viongozi wa mtaa huu kusimamia vizuri miradi hii ili iweze kudumu ili miradi hii iweze kutumika kama ilivyopangwa...

Tumefanya uzinduzi wa miradi hii katika maeneo mengi, kuna kamati za miradi baadhi ya viongozi wa mitaa wameanza kunyemelea miradi hiyo na kuanza kukusanya fedha....

Niwaimize DAWASA, kwa kazi kubwa wanazozifanya za kusambaza maji kuna mradi wa Maramba mawili tunahakikisha wanapata Maji na hivi katibuni watapata Maji."amesema Makori 

Naye Diwani wa Kata hiyo Haruni Mdoe amesema wakati anagombea nafasi  hiyo,kero kubwa kwa wakazi wa kata hiyo ilikuwa kukosekana kwa huduma ya majisafi na salama. 

Mdoe amesema hata hivyo kwa kuwa ipo kwenye ilani ya Chama Tawala cha Mapinduzi (CCM) ya  kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama aliamini itatatekelezwa wakati uliopangwa na Serikali. 

"Ilikuwa ni changamoto  kubwa lakini jambo la kufurahisha ni kwamba hadi sasa Kata hii yenye mitaa tisa umesalia mtaa mmoja tu wa Ukombozi ndiyo haujapata maji, "amesema. 

Amesema kuna kasi ya utekelezaji wa miradi ya wanachi kwa kuwa Serikali imekuwa ikiifuatilia kwa karibu, hivyo hakuna ubabaishaji, umewekwa utaratibu mzuri wa kuwafungia wananchi maji malipo ya gharama yanafuata pamoja na ankara .

Kaimu Mkurugenzi wa Miradi DAWASA, Lidya Ndibalema amewataka wakazi hao kulipia ankara zao kwa uaminifu, ili kuwezesha miradi mingine ya maji katika maeneo mengine jijini haha kutekelezwa. 

"Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi mkubwa wa usambazaji wa maji ambao unagharimu takribani bilioni 79," amesema Ndibalema.

Mmoja wa wakazi hao amesema kero ya kukosa maji imewatesa kwa muda mrefu wamekuwa wakinunua maji yananayouzwa kwenye magari ya watu binafsi, ambapo wakati mwingine hupata mashaka ya usalama  kutokana na radha au mwonekano wake. 

Wakazi wengi walionekana wakiwa kwenye pilika za kutoa nakala za vitambulisho na picha ili kujiorodhesha kwa maofisa wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam  ili waweze kuunganishiwa huduma ya kufungiwa maji kwenye nyumba zao.

Habari Kubwa