DC Mtanda awaonya watumiaji bandari bubu Nkasi

14Jun 2019
Mary Geofrey
NKASI
Nipashe
DC Mtanda awaonya watumiaji bandari bubu Nkasi

MKUU wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, amewataka watumiaji wa bandari bubu katika wilaya hiyo, kuacha mara moja na badala yake kutumia bandari ya Kipili, iliyofanyiwa ukarabati na Mamlaka ya Bandari (TPA) kwa shughuli zote za bandari.

Muonekano wa bandari ya Kipili

Aidha, ameahidi kufanya operesheni maalum kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kuzuia matumizi ya bandari bubu zote zilizopo na zinazofanya kazi katika maeneo ambayo hayajarasimishwa na kuisababisha Serikali kukosa mapato.

Mtanda ameyaeleza hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea bandari ya Kipili ambayo imefanyiwa ukarabati na TPA kwa gharama ya Sh. milioni 430 ikiwamo ujenzi wa eneo la kuegesha magari makubwa na madogo.

"Baada ya uboreshaji huu mkubwa kukamilika, bandari yetu imekuwa ya kisasa, hivyo ni wakati muafaka kwa wanaofanya shughuli za bandari kuanza kuitumia na kuachana na bandari bubu zote zinazozunguka wilaya hii ya Nkasi,"  amesema Mtanda na kuongeza kuwa,

"Natoa wito kwa watumiaji wa bandari bubu zote kuacha kuzitumia mara moja hii bandari inajitosheleza. Tutafanya operesheni maalum kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama tutakaowakamata wanatumia bandari zilizopigwa marufuku tutawachukulia hatua za kisheria."

Akiwa katika bandari bubu ya Kirando, Mtanda amesema TPA wameshabaini bandari bubu 46 zilizopo katika mkoa wa Rukwa na watazirasimisha baadhi na nyingine zitafungwa ili kuongeza ufanisi wa mamlaka.

Awali Meneja wa Bandari ya Kigoma, ambaye anasimamia bandari zote za Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese, amesema bandari hiyo haikuwa na barabara ya kuingia na eneo la kuegesha magari hali iliyokuwa inasababisha usumbufu kwa watumiaji.

Amesema tayari eneo hilo limeshafanyiwa ukarabati hivyo wafanyabiashara na wenye vyombo vya usafiri wanapaswa kuanza kufanya shughuli zao eneo hilo lenye usalama na maofisa wa mamlaka zote zinazozimamia shughuli za bandari.

Aidha, amesema Wakala wa Barabara (Tanroad) wameshajenga barabara ya kuingia katika bandari hiyo, hivyo hakuna changamoto inayowazuia wenye vyombo vya usafiri na wafanyabiashara kuacha kuitumia.

Amesema bandari hiyo awali ilikuwa ikihudumia meli ya MV Liyemba iliyopata ajali mwaka jana katika Ziwa Victorua na kwamba ilikuwa msaada kwa wakazi wa maeneo hayo kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo yao.

Pia amesema biashara kuu inayofanyika katika bandari hiyo ni usafirishaji wa mazao ya nafaka kama mchele, sukari, maharage na mahindi kwenda nchi ya Demokrasia ya Congo.

Naye Msimamizi wa bandari hiyo,Hamis Mselemu, gharama za kusafirisha mizigo zinalingana na zile wanazotozwa wafanyabiashara katika bandari bubu.

Pia amesema tani moja ya mizigo wanatoza Sh. 6,000 hivyo aliwataka wanaotumia bandari bubu kuitumia ya Kibili kwa sababu ina kina kirefu zaidi ya nyingine.