DC ‘kula sahani moja’ na wanaume mafataki

22Sep 2021
Steven William
Muheza
Nipashe
DC ‘kula sahani moja’ na wanaume mafataki

MKUU wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Halima Bulembo, ametoa onyo kwa wanaume mafataki wanaofanya mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wanaosoma katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.

Hivyo, amewataka kuacha mara moja kwa kuwa kiama chao kimefika kwenda jela miaka 30.

Alitoa onyo hilo wakati akizungumza na vijana katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Wilaya pamoja na wafanyabiashara alipotembelea Soko la Nafaka, Soko la Mboga, Soko la Mitumba, Soko la Samaki na Soko la Michungwani, kusikiliza kero na kuzitolea ufafanuzi.

Alisema kuwa kuna matukio mengi katika Wilaya ya Muheza yamekuwa yakijitokeza wanaume watu wazima na vijana kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari na kuwapa mimba.

Bulembo alisema kuwa katika mikoa ya bara kuna wafanyakazi wengi wa ndani kutoka Wilaya ya Muheza kwa sababu ya kukatishiwa masomo na wanaume mafataki.

Alisema kuwa sasa anataka kupambana na wanaume mafataki katika Wilaya ya Muheza wanaofanya mahusiano ya mapenzi na wanafunzi ili iwe fundisho.

Katika hatua nyingine Bulembo alisema kuwa fursa za mikopo ya asilimia 10 ipo kwa ajili ya wafanyabiashara, wajasiriamali kutoka Halmashauri ya Muheza, hivyo aliwataka kuunda vikundi.

Alisema kuwa wafanyabiashara wote wajasiriamali katika Wilaya ya Muheza lazima wakate vitambulisho vya ujasiriamali kwa gharama ya Sh. 20,000 kutoka kwa maofisa watendaji.

Bulembo alisema kuwa serikali inataka kupata mapato kwa ajili ya kutekeleza huduma za kijamii kama vile afya, miundombinu ya barabara, maji, kuboresha masoko, elimu na umeme.

Diwani wa Kata ya Genge, Moze Kisiki, alisema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muheza ameyasikia na kwamba watayafanyia kazi.