DC aeleza chanzo moto uliounguza bweni

24Nov 2020
Na Waandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
DC aeleza chanzo moto uliounguza bweni

SIKU moja baada ya kutokea ajali ya moto uliounguza bweni katika Shule  ya Sekondari ya Wasichana ya Loreta ya jijini Mwanza,  Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Severine Mathias, amesema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.

Kutokana na hali hiyo, amezitaka taasisi mbalimbali kufuata ushauri wa wataalamu wakati wa kujenga majengo makubwa.

Alitoa kauli hiyo juzi shuleni hapo wakati wa ibada maalum iliyowashirikisha wazazi, walimu, wanafunzi na viongozi wengine wa serikali.

Alisema tukio hilo ni baya na linasikitisha, lakini bahati nzuri hakuna  mwanafunzi aliyepoteza maisha katika ajali hiyo ambayo ilitokea Jumamosi usiku.

Mkuu huyo wa Wilaya aliomba  shule zote za bweni na taasisi zinazohudumia wananchi  kujenga kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa  zimamoto na uokoaji ili kuepusha majanga ya moto yanayojitokeza.

Alisema kwa kuzingatia maelekezo ya zimamoto na uokoaji kila jengo lizingatie tahadhari katika kujenga majengo na miundombinu inayokidhi mahitaji pamoja na vifaa vya kudhibiti na kuzimia moto ili kuepusha athari.

Alisema chanzo cha moto katika bweni hilo la ghorofa  tatu ni hitilafu ya umeme kama alivyoelezwa na wataalamu wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Jeshi  la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Aliwaomba wazazi wenye watoto  wanaosoma katika shule hiyo kuwa na amani kwani  hakuna madhara ya kifo yaliyotokea, hivyo wanamshukuru Mungu kwani wakati unatokea moto huo ni wakati watoto walikuwa wanajiandaa kupata chakula, sala kwa kuzingatia ratiba ya shule hiyo ni ya kidini.
 
Aliziomba  taasisi za serikali, binafsi na jamii kwa ujumla kuchangia vitu mbalimbali vitakavyowezesha wanafunzi kusoma na kurudi katika hali ya kawaida ambapo kama halmashauri itachangia baada ya tathmini kufanyika na kujua mahitaji yanayohitajika.

Pina Kiwia, mmoja wa wazazi akizungumza na Nipashe, alisema walivyopata taarifa za kuungua shuleni hapo, walipatwa na mshtuko mkubwa ambao uliwapa  hofu ya kuwapoteza watoto wao ama kujeruhiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, Pastry Massota, alishukuru Mungu kwa kuwanusuru wanafunzi hao na kwamba wanapaswa kusahau yote yaliyopita kwa kuwa  kesho wale wa kidato cha nne wanaanza mitihani yao.

Mmoja wa wanafunzi aliyenusurika katika tukio hilo, Abigael Vincent, alisema baada ya kuuona moto alishuka kwa uharaka chini na kutoa taarifa za moto, hivyo wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwanusuru na janga hilo.

Kwa upande Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Angeline Mabula, alisema matukio kama hayo mara nyingi yanaumiza watoto, wanajeruhiwa au kupoteza maisha.

Aliupongeza uongozi wa shule hiyo, maana ulikuwa umejiandaa kwa tahadhari ya moto kwani ni miezi michache tu walikuwa wamekaguliwa na zimamoto, hivyo alishauri tahadhari iendelee kuchukuliwa  hasa kwenye maeneo ambayo wanakuwapo watoto ili kudhibiti majanga hayo ambayo yanaweza kutokea.

Imeandikwa na Neema Emanuel na Antony Gervas, MWANZA

Habari Kubwa