DC agoma kufungua semina za posho

09Oct 2019
Neema Sawaka
Kahama
Nipashe
DC agoma kufungua semina za posho

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Annamringi Macha, amekataa kufungua au kufunga semina yoyote itakayofanyika wilayani hapa yenye lengo la kulipana posho kwa washiriki wake.

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Annamringi Macha, picha mtandao

Macha alisema hayo juzi wakati akifunga semina ya watoa huduma 36 kutoka katika idara ya afya ya Halmashauri ya Ushetu yeye lengo la kutoa elimu juu ya mfumo wa ukusanyaji taarifa za utoaji huduma za afya na udhibiti wa mapato kwa njia ya elekroniki (GOT-HOMIS).

Alisema kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakiendesha mafunzo mbalimbali kwa lengo moja la kuhalalisha matumizi ya fedha na kujilipa posho jambo ambalo kwa serikali ya awamu ya tano halikubaliki.

“Kama kutakuwa na mafunzo ya namna hiyo yenye lengo la kujipa posho siwezi kuja kabisa na wala mtu asihangaike kunitafuta kwani siwezi kupoteza muda wangu,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema ameamua kushiriki katika semina hiyo baada ya kujiridhisha kuwa malengo yake yalikuwa kutoa elimu ya kielekroniki kwa watumishi wa idara ya afya ambayo ni muhimu katika maisha ya kila siku ya binadamu.

Aliwataka wanasemina hao ambao ni watoa huduma katika vituo vya afya na zahanati, kutambua kuwa wagonjwa wengi katika maeneo ya vijijini hutibiwa katika zahanati na kupona huku akisisiza kuwa hospitali za wilaya au zile mkoa ni za rufani tu.

Macha alisema kuwa hospitali za rufani hupokea wagonjwa walioshindikana ambao hutoka katika zahanati au vituo vya afya ambavyo kwa kiasi kikubwa viko maeneo ya vijijini ambako ndiko kwenye kundi kubwa la wananchi wanaohitaji huduma za afya kwa hali ya juu.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Ushetu, Dk. Nicodemus Senguo, alisema mafunzo hayo ya kutumia kompyuta kwa watumishi wa afya katika zahanati 22 na vituo vya afya vitatu, yatasaidia kuongeza mapato ya halmashauri na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha.

Senguo alisema pia mfumo huo utaboresha utunzaji wa taarifa za wagonjwa na mtiririko wa uingizwaji na utoaji wa dawa kwa wagonjwa.

Aliongeza kuwa Halmashauri ya Ushetu imetumia Sh. milioni 96 kununua kompyuta na kutoa mafunzo kwa watumishi 53 wa idara ya afya walioko katika vituo vya afya na zahanati zilizoko katika halmashauri hiyo.

Habari Kubwa