DC ajitoa mbio kuwania ubunge, Nassari atua CCM

09Jul 2020
Na Waandishi Wetu
Arusha
Nipashe
DC ajitoa mbio kuwania ubunge, Nassari atua CCM

MKUU wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, amesema kwa sasa hana mpango wa kutangaza nia ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika majimbo ya Hai na Arusha Mjini ambako kwa muda mrefu alikuwa akitajwa.

“Mimi leo nimesimama hapa kutoa shukrani kwamba Mungu ametenda maajabu na mimi siwezi kuyaelezea. Ni heshima kusema kwamba hayo yalifanyika (kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya) nikiwa Diwani wa Sambasha na muda wangu umekoma.

"Watu wakikutajataja hata kama siyo wapigakura, wakasemasema, maana yake wanakuambia habari njema kuhusu wewe na niwaambie tu watu wa Sambasha inawezekana wametaja kuhusu Arusha hata hapa, hata huko Hai, lakini nimekuja kuwaambia sitagombea udiwani tena, wala sitagombea ubunge popote," alisema.

Ole Sabaya alisema kwake ni heshima kubwa zaidi, siyo tu kuteuliwa na Rais, lakini kuteuliwa na Rais aina ya Dk. John Magufuli, akikuelezea kuwa ni habari kubwa zaidi.

“Heshima hiyo niliyoitamka hapa, mtu aliyekunyanyua katika kipindi ambacho watu wengine wote hawakuamini na baadaye baadhi ya wale watu wakarudi wakasema unafanya kazi njema, walewale!

"Mimi huyo huyo niamke niende nikatafute nafasi nyingine, kwangu haitakuwa na thamani ya ubunge, ila nitakuwa nimetambulisha kama mtu mwenye uchu na tamaa," alisema.

Alisema ataendelea kuwatumikia wananchi wa Hai hadi hapo Mungu na Rais Magufuli atakapoamua vinginevyo.

Wakati Ole Sabaya akiweka msimamo huo, Mbunge wa zamani wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari, amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akieleza kuvutiwa na juhudi za Rais Magufuli kubadili sura ya Tanzania kimataifa.

“Kweli ninakishukuru chama changu (CHADEMA) kwa kunilea na kunifikisha hapa nilipo, lakini roho yangu inakataa kuendelea kubaki huko na kupinga yanayofanywa na Rais wangu (Magufuli) kama mashamba ya Valeska na Madila na mengine ambayo niliyapigania turudishiwe toka mikononi mwa wawekezaji na Rais ameyarudisha na sasa ni ardhi ya wananchi wa Meru," Nassari alisema jana.

Nassari aliyekuwa ameongozana na Ole Sabaya na kupokewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana CCM Taifa (UVCCM), Kheri James katika Ofisi za CCM Mkoa wa Arusha, alisema kama si Rais Magufuli, suala la Tanzania kutangazwa ulimwenguni kwa sasa kuingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati, ingekuwa ni ndoto.

“Sikuwahi kuwaza kama ipo siku nitatamka 'CCM oyee', lakini baada ya kutafakari kwa muda mrefu, roho yangu inakataa kabisa kubaki upinzani, Rais Magufuli ametekeleza yote niliyoyapigania ikiwamo kurudisha ardhi ya watu wa Meru ambayo nimeipigania miaka yote.

“Roho yangu imeniambia nijiunge na CCM, marafiki walionichangia, ndugu na jamaa wote wamenishauri jambo hili la kujiunga CCM mchana kweupe, kwa sababu ninaipenda nchi yangu na ninaondoka siyo bahati mbaya.

“Ninaomba radhi wale wote watakaokwazika kuniona nimerudi CCM, wanisamehe kwa sababu roho yangu imekataa kubaki upinzani wakati kuna mazuri mengi yanayofanywa na CCM kupitia Rais Magufuli na nimeshaandika barua ya kutaarifu chama changu cha zamani, kuhusu uamuzi huu na nimeambatanisha na kadi yao kuwarudishia,” alisema.
*Imeandikwa na Cynthia Mwilolezi na Godfrey Mushi

Habari Kubwa