DC aonya ndoa za utotoni kipindi cha likizo

26Mar 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
DC aonya ndoa za utotoni kipindi cha likizo

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amewaonya wazazi wilayani humo, kutowaozesha wanafunzi ndoa za utotoni katika kipindi hiki cha mapumziko ya dharula ili kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwang'osha halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Mboneko alibainisha hayo jana wakati alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Mwang'osha, Lyabusalu na Mwiseme, vilivyopo Shinyanga.

Alisema katika kipindi hiki cha likizo wanafunzi wanapaswa kukaa majumbani na kuacha kudhulula hovyo mitaani, ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona, pamoja na kutopata ujauzito, huku akiwataka wazazi kutowaozesha watoto wao ndoa za utotoni.

"Natoa tahadhari kwa wazazi, msiwaozesha wanafunzi ndoa za utotoni katika kipindi hiki cha likizo, na nyie wanafunzi acheni kudhulula hovyo mitaani ili msije kutuletea wapangaji tumboni (mimba), pamoja na kupata maambukuzi vya virusi vya corona, bali bakini nyumbani mjisomee,” alisema Mboneko.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko katikati akikagua uchimbaji wa mtaro wa mabomba katika kijiji cha Mwang'osha.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akikagua mradi wa maji katika kijiji cha Lyabusalu wilaya ya Shinyanga ambao tayari umeshaanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza na baadhi ya wananchi katika kijiji cha Mwiseme Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga alipomaliza kukagua miradi ya maji na ukarabati wa Zahanati.

"Naagiza pia watendaji wa vijiji kipindi wanafunzi watakapofungua shule mfanye ukaguzi wanafunzi gani ambao hawaja kwenda shule, ili tubaini wale waliopewa ujauzito na kuolewa ndoa za utotoni ili tuwabane wazazi wao"aliongeza.

Katika hatua nyingine aliwataka wananchi wa halmashauri hiyo ya wilaya ya Shinyanga, kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji tililika na kutoshikana pamoja na kupiga chafya kwa kujifunika.

Nao baadhi ya wazazi akiwamo Richard Buswege, walisema watatii maagizo hayo ya kutoozesha wanafunzi ndoa za utotoni, pamoja na kuwabana kukaa majumbani na kutodhulula hovyo mitaani.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akinawa mikono kwa kutumia kibuyu chirizi ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi.

Habari Kubwa