DC apiga marufuku uchangishaji lazima madawati

23Jan 2021
Neema Emmanuel
Magu
Nipashe
DC apiga marufuku uchangishaji lazima madawati

MKUU wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Salum Kali, amepiga marufuku walimu wa shule za msingi na sekondari kuwadai watoto michango ya madawati kabla ya kuanza masomo.

Badala yake, amewataka wakuu hao wazungumze na wazazi na walezi kama watakubali kuchangia kwa hiari na si kwa kuwalazimisha.

Kali alitoa agizo hilo jana mjini hapa alipokutana na wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari, waratibu wa elimu wa kata na ofisa elimu wa wilaya katika kikao chao cha kazi.

Alisema serikali haimlazimishi mzazi kuchangia madawati badala yake walimu wanapaswa kufanya mazungumza ya hiari na kirafiki kuwashawishi ili wachangie.

“Ofisa elimu na nyie walimu wakuu msizuie wanafunzi kuanza shule na wale waliofaulu kuingia kidato cha kwanza kuzuiwa kuanza masomo kwa kudaiwa madawati,” alisema Kali.

Aliwataka walimu kutumia mbinu mbalimbali ikiwamo kushirikisha wazazi na wadau wengine kuwaomba wachangie madawati.

Wilaya ya Magu, alisema imekuwa ya pili kwa ufaulu na kwamba lazima watoto wote waendelee kusoma bila vikwazo vyovyote.

"Ukiitumia lugha nzuri kwa wazazi wanaweza kuchangia sehemu kubwa upatikanaji wa madawati na watoto wakaweza kusoma vizuri,” alisema.

Pia mkuu huyo wa wilaya aliwataka  walimu kushiriki kwenye ujasiriamali kwa kuuza mifugo kwenye kiwanda cha nyama kilichoko wilayani Magu.

Aliongeza kuwa hakuna kitu kibaya kama mwalimu kuwa ombaomba na kuweka madeni mtaani badala yake wajitahidi kufanya shughuli za kuwaongezea kipato ili waishi vizuri.

Glory Mtui, Ofisa Elimu Wilaya ya Magu, alisema licha ya elimu kutolewa bure, wazazi bado wana jukumu la kuchangia kwa hiari ili kupata madawati katika shule mbalimbali.

Aliongeza kuwa hakuna mwanafunzi yeyote atakayerudishwa nyumbani kwa kushindwa kuchangia madawati.

Habari Kubwa