DC ataka wananchi wafunzwe sheria za maji

10Dec 2016
MUHEZA
Nipashe
DC ataka wananchi wafunzwe sheria za maji

KATIKA jitihada za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ya mabonde ya mito na kuchafua maji, wakati umefika kwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kutoa mafunzo ya kuelimisha umma ili kufahamu sheria ya maji na mazingira ili watunze vyanzo ya maji.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanasha Tumbo.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanasha Tumbo, alisema hayo juzi wakati akifungua mkutano mkuu wa Jumuiya ya Watumia Maji wa Bonde Dogo la Mto Kihuhwi mjini hapa.

Aliitaka Wizara kutoa mafunzo kwa wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji ili kuwafahamisha masuala ya kutunza mazingira ya vyanzo vya maji.

Aidha alionya kuwa wananchi wanaweza kupigana wakigombea maji lakini Tanzania hataki hilo litokee na kuhimiza viongozi wasimamie sheria ili maji yasipotee na jangwa kutawala

Tumbo alisema kuwa wapo watu wanaoharibu vyanzo vya maji kwa kufanya shughuli mbalimbali kama kilimo, kuchoma mkaa na ufugaji na kutaka wafichuliwe ili sheria ichukue mkondo wake kuzia kuharibu mazingira.

Alisema kuwa hivi sasa kuna upungufu wa maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi na wananchi wanaharibu mazingira katika vyanzo vya maji kwa kukata miti.

Alionya kuwa hata minazi nayo nyakati hizi inakatwa huku akisisitiza wananchi katika vijiji na vitongoji wapande miti na kuitunza.

Mohamed Juma akisoma risala ya watuami maji lya Bonde la Kihuhwi, alisema lengo la mradi huo ni kukabiliana changamoto zinazosababisha uharibifu wa bonde hilo na usimamizi wa vyanzo vya maji .

Alitaja uchimbaji wa madini ndani ya mto, kuchafua maji kwa kufua na kuoga ndani ya mto na kujisaidia mtoni pamoja na kukata miti ovyo kandokando ya mto ni tatizo.

Alisema kilimo kisichozingatia mazingira, ufugaji kwenye mito, kutumia sumu na uchomaji wa moto ni mabo yanayotishia uhai wa bonde hilo.

Juma alisema kuwa kutokana na uongozi uliochaguliwa katika mradi huo kuazimia kupambana na changamoto zilizotajwa, ana imani kutakuwa na mabadiliko.

Aidha aliahidi kuwashirikisha wananchi na wadau wengine ili kwa pamoja washirikiane na vyombo vya dola kudhibiti uhalifu.

Alisema kuwa matarajia yao ni ikushirikiana na Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Mto Pangani ambao ndiyo watakaowasaidia katika jitijhada za kufanikisha utekelezaji bora wa miradi ya usimamizi na uhifadhi wa vyanzo vya maji katika bonde dogo la mto Kihuhwi.

Habari Kubwa