DC awaonya ‘mafataki’ wanaorubuni wanafunzi

29Nov 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
DC awaonya ‘mafataki’ wanaorubuni wanafunzi

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, amewaonya wanaume wilayani humo, kucha tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi.

Amesema kitendo hicho kinasababisha kuzima ndoto za wanafunzi, kwa kuwapatia ujauzito na kuacha masomo, pamoja na kuwaweka katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU).

Mboneko aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, kilele chake kikitarajiwa kufanyika Desemba Mosi, mwaka huu.

Alisema wanaume kufanya mapenzi na wanafunzi ni kosa kisheria, kwa sababu watoto hao hawana uelewa katika matumizi ya kinga.

"Nawaonya wanaume acheni kutongoza wanafunzi, waacheni wasome ili watimize ndoto zao, mtawaharibia maisha kwa kuwapa ujauzito,” alisema Mboneko.

Aidha, aliwataka wananchi kutowanyanyapaa watu ambao wanaishi na maambukizi ya VVU, bali washirikiane nao kufanya shughuli za kiuchumi.

Pia aliwataka watu wanaoishi na VVU kuendelea kutumia dawa za kufubaza makali, pamoja na wahudumu wa afya kuendelea kuwapatia huduma stahiki kwa wakati.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Dk. Damas Nyansira, akisoma taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU wilyani humo alisema yapo asilimia tatu, huku mkoa yakifikia asilimia 5.8.

Habari Kubwa