DC awaonya wafanyabiashara mafuta

09Dec 2018
Robert Temaliwa
BAGAMOYO
Nipashe Jumapili
DC awaonya wafanyabiashara mafuta

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, amewataka wafanyabiashara wa mafuta ya kupikia wanaopitia bandari ya Bagamoyo kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuwafichua wafanyabiashara wanaotumia Bandari bubu kupitisha mizigo yao.

Kawawa alitoa ushauri huo juzi  alipokutana na wafanyabiashara hao wanaopitishia bidhaa zao katika bandari ya Bagamoyo kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Kikao hicho pia kiliwashirikisha maofisa wa forodha, afya, biashara, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA)  na mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika kikao hicho, wafanyabishara hao walilalamikia kukamatwa na askari polisi hali inayosababisha  kukwamisha biashara zao kwa siku kadhaa licha ya kuwa vibali  vimekamilika.

"Tunapata taabu sana na polisi, wanatukamata, wanakuja nyumbani na bunduki mpaka sasa mtoto wangu anaogopa kwenda shule kwa hofu ya polisi. Kwa nini hawatukamati wakati tunatoa mizigo wanatufuata nyumbani?," mmoja wa wafanyabiashara hao,  Shaaban Hamsini, alilalamika.

Kutokana na malalamiko hayo, Kawawa alisema ili kuepuka usumbufu, wafanyabiashara wanaotumia bandari ya Bagamoyo na kulipa ushuru na kodi wanapaswa kuwataja wenzao wanakwepa kulipa kodi za serikali ili washughulikiwe.

Alisema serikali itaendelea kuwasaka wale wote wanaokwepa ushuru na kodi za serikali na kuhakikisha inadhibiti bandari bubu zote zilizopo Bagamoyo.

"Labda niwaambie ndugu zangu, hii kadhia ya kukamatwa kamatwa haiwezi kwisha hapa Bagamoyo kama hamtatupa ushirikiano wa kuwataja wale wote wanaotumia bandari bubu kukwepa kulipa ushuru na kodi za serikali, " alisema Kawawa.

Kawawa amewataka wataalamu kutoka TFDA, TPA na TRA kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao ili kila mmoja aweze kutumia njia sahihi kwa wakati sahihi ili kuepuka usumbufu.

Alisema kila mmoja ana wajibu wa kukomesha bandari bubu kwa kuwa bandari hizo si tu zinapitisha mafuta bali pia  vinaingizwa vitu vya aina mbalimbali ambavyo vingine ni hatari kwa usalama na afya za binadamu.

Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi (SSP) Rajabu Shemndolwa, alisema polisi wanapotekeleza majukumu yao hawana lengo la kumkomoa raia bali wanafanya hivyo kwa kuzingatia sheria na kanuni.

Shemndolwa aliwataka raia wote wilayani hapa kutii sheria bila ya shuruti ili kila mmoja afanye shughuli zake kwa amani na utulivu.

Akizungumzia kukamatwa kwa magari yanayobeba bidhaa zinazotoka bandarini, Shemndolwa alisema hiyo ni katika kuhakiki mzigo uliobebwa kama umefuata taratibu za kisheria kuuingiza.

Aliongeza kuwa polisi ndio wenye mamlaka ya kisheria kusimamisha gari na ukaguzi wa nyaraka mbalimbali za mzigo unafanywa na idara husika ili kujiridhisha kilichobebwa kama kinafanana na nyaraka zilizoonyeshwa.

Shemndolwa alisema tayari ameshatoa maelekezo kwa askari polisi juu ya utaratibu wa kukamata magari yaliyobeba mizigo na kukagua kinachowahusu na maafisa wa idara zingine za serikali watakagua vinavyowahusu ili kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa ufasaha.

Habari Kubwa