DC Chaula afanya maamuzi magumu uandikishaji wapiga kura

17Oct 2019
Godfrey Mushi
SIMANJIRO
Nipashe
DC Chaula afanya maamuzi magumu uandikishaji wapiga kura

UAMUZI wa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zephania Chaula kuhamishia vituo vyote vilivyokuwa katika kata mbili, kwenda lango kuu la kuingilia mgodi wa madini ya ‘Tanzanite’ uliopo Mji mdogo wa Mirerani, umezaa matunda baada ya kuandikisha watu 2,885 ndani ya muda usiozidi saa 10.

Zoezi la uandikishaji wapiga kura likiendelea katika lango kuu la kuingilia kwenye migodi ya tanzanite, Mirerani. PICHA: GODFREY MUSHI

Leo, mamia ya wachimbaji wadogo wa madini maarufu kama 'wanaapolo' walilazimika kupanga foleni kwanza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili kupewa kikaratasi cha kuruhusiwa kuingia migodini kuendelea na shughuli zao.

Kuanzia asubuhi mamia ya wafanyabiashara na wachimbaji wote, walizuiwa katika lango kuu kuingia migodini hadi ili wajiandikishe. 

Akizungumza na Nipashe, Mkuu huyo wa Wilaya amesema, “Lile zoezi pale lango kuu Mirerani, limesaidia sana kwa sababu watu wamejitokeza kwa wingi sana na uzoefu unaonyesha katika siku za mwisho watu ndio hujiandikisha.Tunaweza kufikia lengo la asilimia 100 ambalo tumewekewa la kuandikisha watu 103, 52.

Wilaya hiyo tayari imeshaandikisha jumla ya wapiga kura 90,408 hadi kufikia jana ambayo ni sawa na asilimia 88.

Kuanzia leo katika lango kuu la kuingia migodi ya Mirerani, vituo vyote vya uandikishaji vilikuwa vimehamishiwa nje ya lango hilo na wachimbaji na wafanyabiashara ya madini waliokuwa wameshajiandikisha, ndio waliopewa kikaratasi kinachoonyesha alama ya tiki na kuruhusiwa kuingia migodini.

Alipoulizwa, Katibu wa Chama cha Wachimbaji wa Madini (TAREMA) mkoani Manyara, Tariki Kibwe kuhusu zoezi hilo, amesema siyo kweli kwamba watu walizuiwa kuingia migodini, isipokuwa serikali ilikuwa imeweka utaratibu wa kujiandikisha kwa ajili ya wananchi hao kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiiji na vitongoji.

"Watu wasipotoshe, ni hivi! serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutaka watu wasisimame kuendelea na kazi, ikaleta waandikishaji katika lango kuu ili wajiandikishe pale na kuendelea na shughuli zao.," amesema na kuongeza kuwa;

"Na waliojiandikisha wote waliingia migodini, nadhani ni utaratibu mzuri wa kila mtu kushiriki uchaguzi huo wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji,” amesema Kibwe.

Habari Kubwa