DC Ilala afurahishwa ujenzi daraja la Coco beach

10Oct 2019
Kelvin Innocent
Dar es Salaam
Nipashe
DC Ilala afurahishwa ujenzi daraja la Coco beach

MKUU wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja kutoka fukwe ya Coco kwenda Selander unaoendelea katika fukwe hiyo jijini Dar es salaam na kuridhishwa na ufanyaji kazi wa mkandarasi aliyepewa kazi hiyo.

MKUU wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema.

Akiwa katika eneo  la mradi huo leo Oktoba 10, 2019, amesema ametembelea mradi huo ili kukagua na kujionea kazi ya ujenzi inavyoendelea pamoja na kusikiliza changamoto wanazokutana nazo katika ujenzi huo.

"Nimefurahi kuona wajenzi wako mbele ya muda kwa asilimia 2 kwa hiyo, inatupa matumaini kwamba daraja letu litamalizika kwa muda ule uliotakiwa au hata kabla ya muda huo," Amesema Mjema.

Ameongeza kuwa suala la usalama katika eneo la kazi hasa kwa mafundi pamoja na watu walio karibu na eneo hilo ambao wanafanya shughuli za kibiashara ikiwamo uvuvi wanataakiwa kuwa makini na kuchukua taadhari ili wasipate madhara.

“Usalama tunaouongelea hasa ni kwa majirani zetu, wanaovua samaki wasiwe wanapita chini ya daraja kwenda kuvua samaki ni hatari vyuma vinaanguka uko chini wanaweza kuwakanyaga na hata mafundi nao wanapaswa kuwa makini kwani ni hatari na kwao.,” Amesema na kuongeza kuwa;

“Kuna watanzania ambao wanafanya kazi takribani 400, ambao wamefaidika na daraja hili na tumshukuru sana Rais John Magufuli, kwa sababu alisema daraja hili litakapo kuwa linajengwa watu wengi watapata faida na fursa ambazo ziko hapa. Na tunaendelea kumpongeza kwa kuwapatia ajira wananchi wake.” Amesema

Habari Kubwa