DC Jokate awahakikishia Waislamu msikiti wa kisasa

12Aug 2020
Romana Mallya
Kisarawe
Nipashe
DC Jokate awahakikishia Waislamu msikiti wa kisasa

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, amewahakikishia Waislamu wilayani humo kuwa ujenzi wa msikiti wa kisasa wa Wilaya wa ghorofa mbili unajengwa kwa sababu huduma ambazo zitatolewa hapo zitasaidia kupambana na umaskini, ujinga na maradhi.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo (aliyevaa hijjab ya bluu), akikagua eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani juzi, shughuli ambayo ameahidi kuisimamia kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ili ndani ya mwaka mmoja ujenzi huo uwe umekamilika. Wengine ni viongozi na waumini wa dini hiyo. PICHA: ROMANA MALLYA

Akizungumza na waumini wa dini hiyo juzi wilayani humo ambao wamemuomba awe mlezi, Mwegelo alisema katika maisha yake hakuwahi kufikiria kupewa heshima kubwa ya ulezi na kuahidi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wake.

Ujenzi wa msikiti huo hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Sh. milioni 500.

Mwegelo aliahidi kusimamia ujenzi huo unaotarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja na kuwaeleza kuwa, anaamini hakuna kitakachoshindikana na tayari ameanza kuzungumza na wadau wa ndani na nje ili kusaidia ujenzi huo.

Alisema msikiti huo utakapokamilika utabeba taswira ya wilaya hiyo ya Kisarawe.

"Katika maisha yangu sijawahi kufikiria kuna siku moja nitapata heshima ya kuwa mlezi wa msikiti na kuombwa kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa msikiti lakini wananchi wa Kisarawe mmenipa heshima hii ambapo ninaahidi sitawaangusha na nitashirikiana nanyi bega kwa bega hadi msikiti ukamilike," alisema.

Alisema atahakikisha wanafanikisha ujenzi wake ili uwe taswira ya misikiti mingine ndani ya wilayani humo.

"Tunafahamu msikiti ni taasisi inayojishughulisha na mambo mbalimbali ya kimaisha katika jamii ikiwa ni pamoja na shughuli za maendeleo, kiuchumi na kiutamaduni na kwa mantiki hii ni jambo muhimu katika kuratibu utekelezaji wa shughuli hizo, tunaamini
huduma ambazo zitatolewa na msikiti huu zitasaidia katika kupambana na umasikini, ujinga na maradhi na wananchi na taifa kwa ujumla litasonga mbele," alisema.

Alisisitiza kuwa maandiko Matakatifu ya Quraan yanaeleza Mwenyezi Mungu humpenda mja wake anayejituma katika kufanya kazi, hivyo akiwa mlezi wa kamati iliyoundwa kushughulikia ujenzi huo atajitajidi kadri atakavyojaaliwa kutoa mchango wake wa hali na mali kufanikisha ujenzi huo mkubwa na wa kihistoria.

"Sote tunafahamu kwamba tuko kwenye kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, ninatoa rai kwenu, dini zote na wananchi wote kuzingatia amani na utulivu. Sitarajii uvunjifu wa amani ndani ya Wilaya ya Kisarawe.

"Ninasema haya nikiamini viongozi wa dini ndiyo walezi wetu mpo karibu na jamii, tuwasaidie vijana watulie, uchaguzi ufanyike kwa usalama na kisha tuendelee na majukumu yetu ya kuijenga Kisarawe.

Katibu wa msikiti huo , Mohamed Bakari alisema kwamba wazo la ujenzi wake ulianza mwaka 2000 na eneo lilipatikana mwaka 2006 na ilipofika mwaka 2007 wakapata ramani na ujenzi wa msingi ulianza mwaka juzi.

"Tulianza kuchangishana fedha kupitia michango ya waumini wetu na katika kipindi cha miaka 10 tukafanikiwa kukusanya Sh.milioni 45 lakini ili msikiti huu ukamilike kama ramani ilivyo, tunahitaji kupata zaidi ya Sh.milioni 500.

Habari Kubwa