DC Jokate awapa kazi maalumu vijana 150

07Aug 2020
Romana Mallya
Kisarawe
Nipashe
DC Jokate awapa kazi maalumu vijana 150

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, amewataka vijana 150 wanaopewa mafunzo ya akiba wilayani hapa, kutoa taarifa za kikundi au watu wanaohamasisha kuvuruga amani ya nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Mwegelo alitoa agizo hilo jana wilayani hapa alipofungua mafunzo hayo ya miezi minne kwa vijana hao ambao miongoni mwao wanawake ni 62 na wanaume ni 88 wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 25.

Mwegelo alisema lazima vijana wawe walinzi wa nchi yao kwa kuweka uzalendo mbele badala ya kuwa sehemu ya kurubuniwa.

"Kuna watu wanalilia amani tuliyonayo Tanzania, kamwe msiruhusu mtu awapotoshe mkahamasika kufanya vitu vya kipuuzi na kuharibu amani ya nchi," aliagiza.

Mwegelo alisema vyombo vya ulinzi na usalama wilayani hapa watafuatilia yoyote atakayejaribu na watamshughukilia kisawasawa na kuwataka vijana hao wasiwe sehemu ya kurubuniwa.

"Tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, mkisikia mtu anayehamasisha kuvuruga amani ya nchi yetu, toeni taarifa, mkawe masikio na macho ya viongozi huko mtaani, kama kuna kikundi au watu wanataka kufanya kinyume, toeni taarifa kwa viongozi," aliagiza.

"Utii, uaminifu, uzalendo na uhodari, kama hizi sifa hauna, hata usome shahada zote ndani na nje ya nchi, utakuwa hufai katika jamii. Mtii serikali na mkawe raia wema, mkalinde rasilimali za taifa na kuzihifadhi, ninategemea hadhi ya uraia wenu itapanda kwa uaminifu mtakaouonyesha baada ya mafunzo haya."

Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Kisarawe, Meja Mohamed Wawa, alisema mafunzo hayo wakati yanaanza, yalikuwa na jumla ya vijana 158, lakini watano walikutwa na matatizo ya kiafya na watatu ni watoro.

Alisema vijana hao hawajawekwa kambini, bali wamekuwa wakiendelea na mafunzo wakitokea nyumbani.

Alisema hayo moja ya malengo ya mafunzo hayo ni kuwaandaa vijana kuwa wazalendo kwa nchi yao na kuwa sehemu ya utoaji wa taarifa kwa mambo ambayo yako kinyume cha sheria za nchi.

Alisema kati ya vijana 150 wanaoendelea na mafunzo, 50 hawana vyeti vya kuzaliwa, tatizo ambalo Mkuu wa Wilaya, Mwegelo aliahidi litatatuliwa, akimwagiza Katibu Tawala wa Wilaya kulishughulikia.

Habari Kubwa