DC Kinawiro aagiza Shule zote kuwekewa mitego ya radi

20Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Bukoba
Nipashe
DC Kinawiro aagiza Shule zote kuwekewa mitego ya radi

​​​​​​​MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Solomon Kimilike, ameagizwa kutafuta pesa kwa ajili ya kuweka mitego ya radi kwenye Shule zote za Msingi na Sekondari,  na katika Ofisi za taasisi za umma, ili kupunguza madhara yatokanayo na radi, ikiwa ni pamoja na kuzuiza vifo vya wanafunzi.

Mkuu wa Wilaya Bukoba Deodatus Kinawiro.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Deodatus Kinawiro, katika kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya hiyo, siku chache baada ya mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari ya Kabugaro iliyoko tarafa Bugabo, Gisera Osward kupigwa na radi na kupoteza maisha papo hapo akiwa shuleni.

"Radi karibu Wilaya nzima ya Bukoba ni tatizo, natoa maelekezo kwako Mkurugenzi, kwa kushirikiana na baraza lako la madiwani tafuteni fedha popote haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kununua mitego ya radi, ili iwekwe kwenye shule zote za msingi na sekondari pamoja na ofisi za taasisi za umma, ili tuweze kunusuru maisha ya watoto wetu" amesema DC Kinawiro.

Aidha, Kinawiro amesema tukio la mwanafunzi kupigwa radi na kupoteza maisha akiwa shuleni limemshtua ingawa sio la kwanza yamekuwa yakitokea mara kwa mara, na kwamba suala hilo lisipochukuliwa kwa uzito zaidi watoto wengi wataendelea kupotea na wengine kupata ulemavu.

Habari Kubwa