DC Lalika ataka wananchi kuwa na mtazamo chanya juu ya elimu ya afya

22Jan 2021
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
DC Lalika ataka wananchi kuwa na mtazamo chanya juu ya elimu ya afya

MKUU wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Severine Lalika amewataka wananchi kuwa na mtazamo chanya juu ya elimu inayotolewa na maofisa wa afya sehemu mbalimbali ikiwamo maeneo ya uvuvi ili kupunguza idadi ya watoto wanaojihusisha na shughuli hizo.

Amesema kuwa katika maeneo ya mialo ya samaki, upasuaji mbao ,madini na masoko ni hatari hasa kwa watoto kwani kumeshamili starehe na kupelekea ongezeko la watoto, mimba zisizotarajiwa na maradhi mbalimbali ikiwemo Ukimwi.

Amesema kuwa wataalamu wa afya Wilaya ya Ilemela  wameweka ratiba ya uhamasishaji wa masuala ya afya na wanafanya mara kwa mara katika kata zote 19 zilizopo wilayani humo hasa kwenye maeneo ya mialo.

"Hizo hali zinawapelekea watoto wetu wa kiume na kike hata wale ambao wapo kwenye umri wa kwenda shule kupenda kujihusisha na shughuli za uvuvi na wakiwa huko wanakutana na adha mbalimbali kwa kuwa hawajafikia umri wa kujitambua na kujikinga kiafya,"amesema Dk Lalika.

Ameelezea kuwa utoro wa watoto shuleni umeshamili hasa katika maeneo zinapofanyika shughuli za uvuvi ambapo unaweza kukuta mtoto wa darasa la pili,tatu na nne, wamekuwa watoro wa kudumu na ufatiliaji ukifanyika mara nyingi wanapatikana katika maeneo ya mialo hivyo aliwataka wakazi wa maeneo hayo kushirikiana na serikali kuhakikisha watoto hao wenye umri wa kwenda shule hawashiriki kwenye shughuli zozote katika maeneo hayo.

" Kuna kisiwa kinaitwa Bezi,Igombe na Makobe huko ukienda kuna starehe ambazo ukiambiwa huwezi kuamini maeneo kama hayo yanamadhara kiafya," ameeleza Dk Lalika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Butuja, Kichonge Mwita amesema elimu inatolewa kwa sasa wakishirikiana na muudumu wa afya ngazi ya Mtaa katika mwalo uliopo katika mtaa wake.

 "Tumetoa elimu ya uzazi kwa kushirikiana na wahudumu afya ngazi ya mtaa tumewafikia wananchi wengi na hivi karibuni tuliitisha mkutano wa hadhara ili kuwapa elimu na maelekezo mwanzo hali ilikuwa ya hatari lakini kwa sasa kidogo mambo yanaleta matumaini" amesema Mwita.

Habari Kubwa