Mboneko amechukua uamuzi huo leo wakati akiongoza kikao cha kujadili kuhusu tukio hilo lililotokea jana katika hospitali hiyo la Askari wa Suma JKT kumchapa mikanda Daudi Lefi, wakati alipokuwa akimuuguza mama yake katika Hospitali ya Rufaa kwa madai amezidisha muda wa kuona wagonjwa.
Mboneko amesema viongozi wa serikali waliona taarifa ya tukio kupitia mitandao ya kijamii. na kuanza kuchukua hatua mara moja ili kubaini ukweli kuhusu tukio hilo ambapo amevipongeza na kuvishukuru vyombo vya habari vilivyoripoti kuhusu tukio hilo na kuagiza Askari wote wa Suma JKT ambao wanalalamikiwa waondolewe wote Hospitalini hapo.

“Tumeona tukio hili kupitia mitandao ya kijamii, kama uongozi wa serikali hatukufurahishwa na jambo hili,baada ya kuona tukio hili tulianza kupata ufafanuzi kutoka hospitalini lakini pia nilimuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kufuatilia tukio hili ambapo tayari hospitali walikuwa wameshaanza kuchukua hatua.”amesema Mboneko na kuongeza;
“Serikali inakemea jambo hilo na isingependa kuona linaendelea mahali popote penye hospitali zetu, zahanati na vituo vya afya na sehemu zingine na kwamba serikali inataka watu wapate huduma nzuri hospitalini, na askari huyu wa Suma JKT, Geofrey Paulo nimeagiza aondolewe hapa Hospitali,”ameongeza.

Meneja wa Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT Guard Kanda ya Ziwa, Kepteni Manika Kihiri, amesema mara baada ya kutokea kwa tukio hilo,hatua za awali walizochukua ni kumuondoa mlinzi huyo eneo la hospitali na kwamba watatekeleza maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwani Suma JKT haipo kwa ajili ya kuzua taharuki katika jamii bali ni kuleta amani katika jamii.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Nuru Mpuya amesema tukio hilo lilizua taharuki hospitalini na kwamba tayari hatua zimeshachukulia na kuahidi kuwa tukio kama hilo lililofanywa na mlinzi wa kampuni ya walinzi waliyoingia nayo mkataba halitatokea na kwamba wataboresha huduma ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu walinzi hao.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga, Dkt. Luzila John Boshi. amesema uongozi wa hospitali umesikitishwa na tukio hilo na kwamba kinachofuata ni kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko.

Jana katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga majira ya saa moja jioni, Daudi Lefi, ambaye alikuwa akimuuguza mama yake kwenye hospitali hiyo, alipigwa mikanda na Mlinzi wa Suma JKT, Geofrey Paulo, akidai kuzidisha muda wa kuona wagonjwa wakati aliporudi wodini kufuatilia jina la mama yake baada ya kutoonekana kwenye kompyuta.
Akisimuliza tukio hilo Dada wa mahanga huyo, Lidya Lefi, amesema baada ya kaka yake kurudi wodini ndipo walinzi hao wa Suma JKT wakamzuia kuingia na alipoingia wakamtoa nje kwa nguvu ndipo mmoja akavua mkanda na kuanza kumchapa nao sehemu mbalimbali za mwili wake.
Naye Daudi Lefi, amesema aliumia sehemu mbalimbali za mwili wake hasa kwenye mkono wa kushoto ambao umevimba na kuchanika kwenye kiwiko.