DC Mfune asisitiza wafanyabiashara kulipa kodi

21Feb 2021
Dotto Lameck
Mbeya
Nipashe
DC Mfune asisitiza wafanyabiashara kulipa kodi

MKUU wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Reuben Mfune, amewaambia wafanyabiashara wa Wilaya hiyo kuwa ni vigumu kutengenisha kodi na maendeleo kwani maendeleo ya nchi yoyote ile duniani hutegemea kodi.

Mfune amesema hayo wakati wa semina ya wafanyabiashara kufuatia kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambayo imelenga kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusu kodi, kusikiliza changamoto zao za kikodi na kupokea maoni kwa ajili ya kuboresha huduma za TRA. 

“Kodi huiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo hapa nchini, kwa mfano ujenzi wa barabara za lami, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa zahanati na ununuzi wa dawa na mengine mengi, yote haya yanatekelezwa kwa kutumia kodi zinazolipwa na ninyi wananchi, amesema Mfune. 

Aidha, Mfune amewasisitiza wafanyabiashara hao kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari na kutumia vizuri mashine za kielektroniki za kutolea risiti kwa kutoa risiti kila wanapouza bidhaa na huduma mbalimbali.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wilayani humo, Michael Mwaiteleke, amesema kuwa, kampeni hii licha ya kutoa elimu ya kodi lakini pia inajenga urafiki kati ya wafanyabiashara na TRA na hivyo itapelekea kuongeza uhiari wa ulipaji kodi nchini.

Habari Kubwa