DC Mwaisumbe ataka watumishi wa forodha kishirikiana

03Jul 2019
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe
DC Mwaisumbe ataka watumishi wa forodha kishirikiana

SIKU chache baada ya Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe kwa kushirikiana na Jeshi la polisi mpaka wa Namanga kukamata madini zaidi ya kilo 36 ya aina tofauti yaliyokua yakitoroshwa kuelekea nchi jirani ya Kenya,-

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe.

-ametoa wito kwa wafanyakazi wa kituo cha forodha upande wa Tanzania ( OSBP) kufanya kazi kwa kushirikiana.

Mwaisumbe amesema kituo hicho kinafanya kazi  kwa masaa 24 kwa kutoa huduma kwa wageni wanao ingia nchini na hata wale wanaokwenda nje ya nchi pamoja na huduma kwa wafanyabiashara mbalimbali wanaopita katika mpaka wa Namanga.

" Kikao hiki ni kikao cha kutathimini kazi zinazofanyika katika kituo hiki cha pamoja na kupanga mikakati mipya ya mwaka wa fedha pamoja na kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa ipasavyo.. Hapa kuna idara 14 na idara zote zinafanya kazi kwa kushirikiana hii yote ni kurahisisha shughuli za watu wanaotumia mpaka huu," amesema Mwaisumbe

Aidha ameeleza kuwa kuna changamoto kwa baadhi ya idara ikiwemo upungufu wa watumishi na vifaa hivyo ameahidi kushirikiana na Wizara zenye dhamana  na pamoja na ngazi ya mkoa kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa ili kurahisisha shughuli katika mpaka huo.

" Serikali inafanyakazi kubwa sana na hata sasa kuna idara hapa zimepata vifaa ikiwemo idara ya mionzi mmeletewa kifaa hapa usumbufu wa kwenda Dar-es-Salaam kupeleka bidhaa sasa hakuna hayo mengine tutayatatua msiogope fanyeni kazi kwa bidii" amesema Mwaisumbe

Hata hivyo amepongeza idara ya mapato TRA chini ya Afisa Mfawidhi katika kituo hicho, Paul Kamukuru kwa makusanyo mazuri yaliyovuka lengo kwa mwaka wa fedha ulioisha  2018/2019 na kuwataka kuhakikisha kasi ya ukusanyaji wa mapato inazidi kukua.

" Hongereni kwa makusanyo mlitakiwa kukusanya shillingi billioni 52 lakini mmekusanya billion 54 nafikiri kama si mvutano baina ya TBS na KEPS mngekusanya zaidi ya hapo nashukuru pia serikali imetatua mgogoro wa idara hizo sasa shughuli zinaendelea bila usumbufu," amesema Mwaisumbe

Mkaguzi wa usalama wa mionzi, Namanga (OSBP) Fadhili Msumali, ameeleza kuwa Idara hiyo inafanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni zake juu ya udhibiti wa vyakula vinavyotumika na binadamu pamoja na wanyama, mbolea zikiwemo bidhaa za mionzi zinazoingia nchini na kutoka.

Alisema kwa sasa Biashara imerahisihwa kwani hapo awali walikua wakilazimika kuchukua sampuli ya bidhaa kuipeleka mkoani Arusha kukaguliwa ,lakini kwa sasa kifaa cha kukagua kimeletwa kipo mpakani hivyo wanakamilisha taratibu zote katika kituo hicho na mwitikio ni mkubwa kwa wafanyabiashara

"Serikali imefanya maboresho kwa kurahisisha shughuli za kibiashara na sasa vifaa vya maabara vinapatikana hapa mpakani "alisema Msumali

Naye Afisa mfawidhi Ukaguzi na uthibiti Wa utoroshaji wa Madini Mpaka Wa Namanga (OSBP) Anorld Kishashu alisema,kitengo hicho kilianza kufanya kazi Mpakani mwaka 2017 hapo awali walikua wakifanya kazi eneo la longido katika kituo cha polisi kwa kukagu magari yanayoenda kenya kama yamebeba madini bila kufuata taratibu (kutorosha).

Amekemea kitendo cha baadhi ya Watanzania kukosa uzalendo na kuendelea kutorosha madini kwa njia za panya kupeleka nchini Kenya huku serikali ikiwa imetengeneza mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wa madini kwa kufungua masoko ya madini na kupunguza baadhi ya tozo za Madini.

" Mwaka 2017 tulikamata madini yenye thamani ya dola 68 yakitoroshwa kwenda Kenya kwa mwaka 2018/2019 tumekamata kg 63 zenye thamani ya shilling billion 1 na zaidi na madini mengi ni aina ya Vito ( Rubi)" amesema Kishashu.