DC Same atoa siku saba kumaliza migogoro ya wakulima,wafugaji

29Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Same
Nipashe
DC Same atoa siku saba kumaliza migogoro ya wakulima,wafugaji

MKUU wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, Edward Mpogolo, ametoa siku saba kwa viongozi wa vijiji na vitongoji kutatua kero za migogoro iliyopo kati ya wakulima na wafugaji badala ya kuziachia mamlaka zingine.

Mpogolo ametoa maagizo hayo leo Julai 29, 2021 baada ya kukutana na malalamiko mengi ya migogoro hiyo wakati akiwa katika ziara yake ya kusikiliza kero za Wananchi katika Kata ya Ruvu na Njoro wilayani humo.

Amesema kukosekana kwa mahusiano na uwajibikaji wa viongozi hao wa ngazi ya chini, kumesababisha mrundikano mkubwa wa kero za wafugaji na wakulima.

"Ni aibu kuona mkulima analalamika kuwa mifugo imekula mazao yake na ameripoti kwa uongozi wa eneo husika lakini hakuna utekelezaji”

“Hii sio picha nzuri hata kidogo kwa viongozi mlioaminiwa na kupewa ridhaa ya kuongoza Wananchi hii inaonyesha hakuna mahusiano mazuri miongoni mwetu. Siwezi kulifumbia macho maana ni aibu." amesema Mpogolo.