DC Shinyanga ampa mwalimu zawadi kwa kupunguza ufaulu wa 'F'

16Jun 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
DC Shinyanga ampa mwalimu zawadi kwa kupunguza ufaulu wa 'F'

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, amempatia zawadi ya fedha Shs. 50,000 pamoja na kiti na meza, mwalimu mwenye ulemavu wa miguu wa shule ya Sekondari Ngokolo Ernest Mpanda, kutokana na kupunguza daraja 'F' kwenye matokeo ya mtihani kidato cha nne 2020.

Mboneko ametoa zawadi hizo leo, wakati akikabidhi meza 12 na viti viwili, kwa ajili ya matumizi ya walimu katika shule ya sekondari Ngokolo, ili kuwaondolea adha ya kutumia viti na meza za wanafunzi.

Amesema amempatia zawadi Mwalimu huyo, kutokana na juhudi zake ambazo anazifanya, huku akiahidi kuendelea kutatua changamoto za walimu wenye ulemavu wilayani humo, ikiwamo kuwajengea mazingira rafiki ya kufundishia na miundombinu ya choo.

"Nimefurahishwa sana na mwalimu huyu kwa kufundisha vizuri wanafunzi na kupunguza daraja F shuleni hapa, na imani katika matokeo ya kidato cha Nne 2021 hakutakuwa na F kabisa," amesema Mboneko.

Naye mkuu wa shule hiyo, Malale Masali, amesema mwalimu huyo licha ya hali aliyokuwa nayo, ndiyo amekuwa mkombozi shuleni hapo kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata ufaulu wa daraja la juu.

Amesema katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019, kulikuwa na F 23 shuleni hapo, lakini alipambana kufundisha na kuzipunguza na matokeo ya mwaka jana zikapatikana F 9.

Naye makamu mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Eliaremisa Mbise, amewataka wazazi kutowabeza watoto wenye ulemavu na kuwaficha ndani bali wawapeleke shule ili watimize ndoto zao ili waje kuwa msaada mkubwa ndani ya taifa.

Naye, Mwalimu Ernest, amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kuwajali walimu wenye ulemavu na kuahidi kutomwangusha kwa kuhakikisha anaifuta 'F' kabisa shuleni hapo.

Habari Kubwa