DC: Tunafanyia kazi madai viongozi Chadema kutekwa

10Jul 2019
Enock Charles
Nipashe
DC: Tunafanyia kazi madai viongozi Chadema kutekwa

MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Miraj Mtaturu, amesema kuwa ofisi yake imeyasikia madai ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu viongozi wao kutekwa na kwamba inayafanyia kazi-

-lakini amekanusha kuhusika kuwasaidia vijana wa ulinzi wa Chama Cha Mapinduzi (green guard) kufanikisha utekwaji wa viongozi hao.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Mkuu huyo wa Wilaya
alibainisha kuwa ofisi yake imeyasikia madai hayo ya Chadema na kuwa inayafuatilia kupitia kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kubaini ukweli wake.

“Kuhusu green guard labda ungemuuliza katibu wa Chama Cha Mapinduzi kwa sababu mimi nafanya kazi yangu kama mkuu wa wilaya na hayo…masuala tumeyasikia na tunachukua hatua ungempata RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) angekwambia
hatua zilizochukuliwa,” Mtaturu alisema.

Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Switbeth Ngiwike kuhusiana na madai ya Chadema ambaye aliahidi tangu juzi kuwa angelitolea ufafanuzi suala hilo, lakini alisema kwa sasa anashughulikia msiba uliotokana na ajali ya gari ya barabarani mkoani humo lililopelekea vifo vya wafanyakazi watano wa Azam Media.

“Lile bwana mniache, mimi nina shughulika na hili suala kubwa la msiba sasa hivi,” Njewike alisema.

Jumapili Chadema kilidai, kutekwa na kuteswa kwa baadhi ya viongozi na wanachama wake Jimbo la Singida Mashariki na vijana wa ulinzi wa CCM (Green guard) katika Jimbo hilo.

Katibu wa chama hicho Kanda ya Kati, Idd Kizota alidai viongozi hao walikuwa katika ofisi za chama hicho katika jimbo hilo katika kikao cha ndani kwa lengo la kufanya uhaguzi wa ndani ya chama, na baadae kuvamiwa na vijana hao na viongozi wao wawili kutekwa na kupelekwa kusikojulikana .

“Walikuwa kwenye uchaguzi wa ndani ya chama katika ofisi ya chama na baadae walivamiwa na kikundi cha vijana wa green guard na kutokomea kusikojulikana na pia walivunja kioo cha gari yetu moja aina ya Ford Ranger, ingawa dereva alifanikiwa kuwakimbia,” Kizota
alisema.

Viongozi wanaodaiwa kutekwa na kuteswa ni Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Singida Mashariki, Agnesta Lambat na Diwani wa Misughaa, Jumanne Rajab ambao kwa mujibu wa Katibu huyo, Agnesta alilazwa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, huku Diwani akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Makiyungu mkoani Singida.

Akizungumzia madai hayo ya viongozi wa Chadema Jumapili, Kamanda Ngiwike alidai anashangaa madai hayo ya watu kutekwa na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litatoa taarifa kuhusiana na suala hilo Jumatatu.

“Hii lugha ya kutekwa kutekwa kutekwa sijui inatoka wapi tutatoa taarifa kesho (Jumatatu) kuhusiana na hilo,” Kamanda Ngiwike alisema.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, alitangaza ratiba ya kufanyika kwa uchaguzi katika jimbo la Singida Mashariki Julai 31 mwaka
huu .

Jaji Kaijage alisema fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya Julai 13 na 18, mwaka huu na uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 18, na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Julai 19 hadi 30.

Uchaguzi huo ni kwa ajili ya kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu (Chadema), ambaye alivuliwa wadhifa huo na Spika wa Bunge, Job Ndigai, kwa maelezo kuwa amekosa sifa.

Habari Kubwa