DCI afunguka mazito

09Jan 2017
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
DCI afunguka mazito
  • • Kutoweka Msaidizi wa Mbowe
  • • Yaliyojiri miili saba ya Mto Ruvu

KAIMU Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz, amefunguka na kueleza juu ya uchunguzi wa madai ya kupotea kwa Bernard Saanane, Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na miili saba iliyoopolewa kwenye Mto Ruvu.

KAIMU Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz.

Mbali na madai ya kupotea kwa Saanane, Kamishna Boaz pia amezungumzia kuhusu mambo mbalimbali yanayoihusu ofisi yake hiyo mpya na changamoto zinazoikabili.

Katika mahojiano mahususi na Nipashe jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema ofisi yake inaendelea na uchunguzi kuhusiana na madai ya kupotea kwa Saanane huku akibainisha kuwa wamekuwa wakipata taarifa mbalimbali juu ya mfuasi huyo wa Chadema.

"Katika hili (la Saanane), tumekuwa tukipata taarifa mbalimbali, na kila taarifa tunayoipata tunaichunguza kuona inatusaidiaje ili kujua kwamba Ben Saanane yuko wapi," alisema.

Saanane anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Kwa mujibu wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mwanasheria
Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, Saanane aliwasiliana kwa mara ya mwisho na Mbowe Novemba 14, mwaka jana na simu yake haipatikani na hajulikani aliko.

Akizungumzia kuhusu miili ya watu saba iliyoopolewa Mto Ruvu, Kamishna Boaz alisema wanaendelea na uchunguzi lakini hawajapata ushahidi au mtu yeyote ambaye ameitambua miili hiyo wala wa kujitokeza na kusaka ndugu zake wamepotea kwa wingi huo.

Desemba 6, mwaka jana, miili hiyo ilikutwa ikielea kando mwa mto huo, kila mmoja ukiwa umefungwa ndani ya mfuko wa sandarusi iliyoshonwa juu na kufungwa jiwe kubwa.

Kamishna Boaz pia alizungumza mambo mbalimbali ya kuyashughulikia katika nafasi yake mpya na namna alivyojipanga kufanya kazi kwa weledi katika kazi hiyo nyeti.

Yafuatayo ni mahojiano ya Nipashe na Kamishna Boaz yaliyofanyika ofisini kwa DCI huyo jijini Dar es Salaam juzi.

Swali: Hongera kwa kuteuliwa kushika nafasi hii nyeti. Uchunguzi wa miili ya watu saba iliyoopolewa kwenye Mto Ruvu umefikia wapi?

DCI: Kwa ujumla tunaendelea na uchunguzi kama nilivyosema wakati ule (mwezi uliopita). Hatujapata ushahidi au mtu yeyote ambaye ameitambua hiyo miili, na wala hatujapokea mtu yeyote anayesema ndugu zangu wamepotea kwa wingi huo au mmoja mmoja.

Kwa hiyo bado tunaendelea na uchunguzi na bado tunaendelea kukaribisha yeyote anayejua jambo lolote kuhusu maiti hao kwa sababu bado hatujafanikiwa sana kupata mtu yeyote ambaye ametueleza jambo la kutupeleka mbele hata kujua nini kilichowasibu.
Swali: Mlichukua sampuli kwenye miili kwa mujibu wa taarifa yako ya mwezi uliopita. Je, mmebaini nini kuhusu sampuli hizo?

DCI: Sampuli zinapochukuliwa ni lazima zilinganishwe na kitu kingine, aidha ndugu zake na vitu kama hivyo, na ndiyo maana tunasema akijitokeza mtu na kusema labda jamani kuna ndugu yangu alipotea itakuwa inatusaidia sana sisi katika uchunguzi.

Kwa hiyo, tunakaribisha watu ambao watasema walipotelewa na au ilikuwa hivi na vile na itaturahisishia kupata taarifa zaidi wakati tunawahoji.

Swali: Kuna madai ya kupotea kwa Saanane katika mazingira ya kutatanisha ambazo ofisi yako ilisema hivi karibuni kwamba inazifanyia kazi. Mmefikia wapi juu ya uchunguzi huo?

DCI: Bado tunaendelea na uchunguzi, katika hili tumekuwa tukipata taarifa mbalimbali, na kila taarifa tunayoipata tunaichunguza kuona inatusaidiaje ili kujua kwamba Ben Saanane yuko wapi.

Swali: Kamishna, ni muda mrefu sasa umepita tangu kuripotiwa kupotea kwa Saanane. Je, kuna taarifa yoyote muhimu ambayo mmeshapata kuhusu madai ya kutoweka kwake?

DCI: Bado hatujabaini, kama nilivyokueleza tunapokea taarifa nyingi sana kuhusu Saanane na siyo kidogo, lakini kila taarifa tunayoipata tunaipima na kuifanyia uchunguzi, lakini bado hatujapata mwanga mzuri kwa ujumla wake kutoka kwenye taarifa hizo.
Swali: Wahamiaji haramu ni miongoni mwa changamoto kubwa Afrika Mashariki kwa sasa. Mmejipangaje kupambana na kadhia hii?

DCI: Suala la wahamiaji haramu ni kubwa sana, hasa katika nchi yetu ambayo ina mipaka mipana. Mfano kuanzia Tanga mpaka Mtwara ni kilomita zaidi ya 1,000, ni maeneo machache sana ambayo ni 'official' (rasmi) kupita, lakini sehemu nyingi sana, mtu yeyote anaweza akaingia.

Tuna changamoto kubwa ya namna ya kuzuia wahamiaji haramu wasiingie nchini kutokana na mipaka mipana lakini pia kutokana na kuwapo kwa njia za panya nyingi.

Kwa mfano, Wilaya ya Rombo peke yake ina njia za panya zaidi ya 300, nchi zetu tunapakana na bahari, kwa mfano wavuvi kutoka katika nchi jirani wamekuwa wakitumia mwanya huo wa bahari au maziwa kuingia nchini.

Wanapotumia majahazi ya uvuvi, kwa mfano, inakuwa rahisi kwao kuingia nchini, lakini tunachokifanya ni kushirikiana kuona kwamba vyombo vyote vya dola vinashirikiana kwa pamoja; polisi, uhamiaji na vyombo vingine kufanya doria za pamoja.

Pia tunafanya jitihada za kujua mitandao ya usafirishaji wa wahamiaji haramu hao, tunaweza tusizuie kuingia lakini tunapojua mitandao ya wasafirishaji, inakuwa rahisi kwa sababu hao watu hawajileti wenyewe.

Swali: Kwa wingi huo wa njia za panya, kuna athari zozote ambazo zimeikumba nchi?

DCI: Hapana, nchi yetu tuna uwezo mkubwa wa ‘ku-control’ (kudhibiti) mipaka yetu. Suala hili si la Tanzania tu, hata nchi za Ulaya zina tatizo hilo japokuwa zina uwezo mkubwa. Kupambana na hilo inategemea na ‘mechanism’ (mbinu) mliyonayo na hali hii inakuwa ngumu zaidi kwa nchi zinazopakana na bahari, mimi ninajua kwamba tuna uwezo mkubwa wa kutatua hilo.

Ukienda kwa mfano kwenye mipaka ya Zambia na Tanzania, yaani wakati mwingine huwezi kujua uko Tanzania au Zambia, yaani muingiliano wa watu na watu ni mkubwa kiasi kwamba humo humo kuna watu wabaya na wazuri, sasa inategemea nyie mmejiwekea ‘mechanism’ gani ya kupambana na hilo.

Wapo wananchi ambao kwa mfano katika maziwa kwenye shughuli za uvuvi wanakuwa wanafahamiana, kwamba hawa ni Watanzania ama hawa siyo, lakini wakati mwingine wananyamaza hawatoi taarifa.

Elimu kwa wananchi inatusaidia, pale wanapoona jambo waseme na hiyo ni njia inayosaidia pia kupambana nalo. Wakati nikiwa Mkoa wa Kilimanjaro, suala hili la wananchi kutoa taarifa lilisaidia sana.

Itaendelea kesho.

Habari Kubwa